Waziri wa Maji, Mhe. Juma Hamidu Aweso (Mb), ameendelea na ziara yake ya kikazi ya kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maji nchini, ambapo leo Julai 24, 2025 ametembelea na kukagua maendeleo ya Mradi wa Maji wa Miji 28 katika Wilaya ya Mpanda, mkoani Katavi.
Katika ziara hiyo, Mhe. Aweso ameonesha kuridhishwa na hatua za utekelezaji wa mradi huo mkubwa, ambao ni miongoni mwa miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama kwa wakati wote.
Aidha, Mhe. Aweso amesisitiza dhamira ya dhati ya Serikali ya kumtua mama ndoo kichwani kupitia uwekezaji mkubwa katika ujenzi wa miundombinu ya maji, ikiwemo dakio la maji ambalo ni sehemu muhimu ya mradi huo.
Katika hotuba yake, Waziri Aweso amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa msukumo mkubwa katika sekta ya maji, ambapo kupitia uongozi wake, zaidi ya shilingi bilioni 22 zimeidhinishwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu mkoani Katavi pekee.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko, amepongeza jitihada za Serikali kwa kuwekeza zaidi ya shilingi bilioni 65 katika sekta ya maji mkoani humo. Ameeleza kuwa matokeo ya uwekezaji huo yamepelekea kuongezeka kwa kiwango cha upatikanaji wa maji hadi kufikia asilimia 68.5 kwa maeneo ya mijini na asilimia 77.3 vijijini, kutoka chini ya asilimia 60 hapo awali.
Mradi wa Miji 28 unaendelea kuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi, ukiwa ni ishara ya utekelezaji thabiti wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved