Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Bw. Albert Msovela, ametoa maelekezo makali kwa watumishi wa umma wa Wilaya ya Tanganyika, akisisitiza umuhimu wa uwajibikaji, uadilifu, mshikamano na utoaji huduma bora kwa wananchi.
Akiweka mkazo kwenye utawala bora, RAS Msovela amewaagiza Watendaji wa Kata na Vijiji kuhakikisha vikao vya kisheria vinafanyika kila wiki na taarifa za utekelezaji zinawasilishwa kwa Mkurugenzi kwa mujibu wa taratibu. Amesema malalamiko mengi kutoka kwa wananchi yanafaa kutatuliwa katika ngazi hizo za chini ili kupunguza mzigo katika mamlaka za juu.
Amesisitiza pia kuimarishwa kwa ukusanyaji wa mapato ya ndani, akizitaka halmashauri kuongeza kasi ya usimamizi wa vyanzo vya mapato ili kufikia malengo ya mwaka wa fedha na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Akizungumzia mwongozo wa Serikali kuhusu utoaji huduma kwa wananchi, Bw. Msovela amewakumbusha watumishi kuimarisha mahusiano chanya na wananchi kwa kutumia weledi, uwazi na kujenga mtiririko mzuri wa huduma kwa kila ngazi.
"Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameagiza turejeshe tabasamu kwa wananchi, hivyo ni wajibu wetu kujenga mfumo unaorahisisha kuwafikia wananchi katika maeneo yote," amesema RAS Msovela.
Aidha, RAS Msovela amewataka watumishi kutumia kwa umakini makundi ya mawasiliano ya kikazi na kuzingatia uadilifu katika maamuzi na vitendo vyao vya kila siku, akibainisha kuwa umoja na kuepuka majungu ni msingi wa ufanisi katika utumishi wa umma.
Katika hitimisho la maelekezo yake, amezitaka idara za kilimo kuimarisha huduma kwa wakulima kupitia uwepo wa karibu wa Maafisa Ugani mashambani, akibainisha kuwa mashamba ndiyo eneo la msingi la utoaji huduma za kitaalam.
Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi – Sehemu ya Utawala na Rasilimali Watu, Bi. Cresensia Joseph, amewataka watumishi kuwa mfano wa kuigwa katika utendaji wao wa kila siku, akisisitiza nidhamu, uwajibikaji, uaminifu na utekelezaji wa maelekezo ya Serikali. Amesema uadilifu na weledi wa watumishi unajenga taswira chanya ya utumishi wa umma na kuongeza imani ya wananchi.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved