Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Bw. Albert Msovela, jana desemba 02, 2025 alifungua rasmi Baraza la Kwanza la Madiwani Wilaya ya Mlele na kusisitiza kwa kina umuhimu wa kufanya kazi kwa misingi ya uwajibikaji katika kila ngazi ya utumishi. Amesema kuwa serikali inahitaji watendaji wanaotenda kazi kwa uaminifu, kasi, na matokeo yanayoweza kupimika.
Akizungumza mbele ya madiwani na wataalamu wa halmashauri, Bw. Msovela amesema miradi mingi ya kimkakati inatekelezwa wilayani Mlele, hivyo kunahitajika ufuatiliaji makini na usimamizi wenye weledi ili kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana na wananchi wanapata huduma stahiki kwa wakati.

Ameeleza kuwa nidhamu ya kazi, uwazi na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu ni misingi isiyopaswa kupuuzwa, kwani ndiyo inayoimarisha taswira ya serikali na kuongeza imani ya wananchi kwa viongozi wao. Msovela amewataka madiwani kuwa mstari wa mbele katika kusimamia maamuzi ya baraza kwa masilahi ya wananchi, badala ya kutanguliza masuala ya kibinafsi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Mhe. Majid Mwanga, amesisitiza umuhimu wa kudumisha uhusiano mzuri kati ya watumishi wa halmashauri na waheshimiwa madiwani. Amesema kuwa mara nyingi ucheleweshaji wa maendeleo hutokana na ukosefu wa maelewano, jambo ambalo linaepukika endapo pande zote zitajenga mawasiliano mazuri.

Mhe. Mwanga amesisitiza kuwa madiwani na watumishi wanapaswa kufanya kazi kama timu moja, wakiheshimiana na kushirikiana katika kupanga, kutekeleza na kufuatilia miradi ya maendeleo. Amesema kuwa ushirikiano ndio msingi wa kuimarisha utoaji wa huduma, kuongeza ufanisi wa miradi na kuleta matokeo chanya kwa wananchi.

Amehitimisha kwa kutoa wito wa kuondoa tofauti ndogo ndogo za kiutendaji na kuwekeza kwenye majadiliano yenye kujenga, ili wilaya iendelee kupiga hatua na kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita.


Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved