Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, mkoani Katavi, limempitisha Diwani wa Kata ya Sitalike, Mhe. Athumani Juma Fimbo, kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo baada ya kupata kura 13 kati ya kura zote 13 katika uchaguzi uliofanyika leo.

Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Bw. Albert Msovela, ambaye alikuwa mgeni rasmi, amewapongeza madiwani kwa umoja waliouonyesha katika kuchagua uongozi mpya. Aidha, amewahimiza kuhakikisha kuwa katika kutekeleza majukumu yao, wanazingatia kanuni, taratibu na sheria ili kuongeza ufanisi na kuimarisha utawala bora ndani ya Halmashauri.

“Niwaombe madiwani mhakikishe mnazingatia kanuni, taratibu na sheria katika kila hatua ya utendaji wenu. Ushirikiano kati yenu na watumishi wa Halmashauri ni msingi muhimu wa kuleta maendeleo kwa wananchi.” Amesema Bw. Msovela.
Aidha, Bw. Msovela amewataka waheshimiwa madiwani kuhakikisha wanasimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo ndani ya Halmashauri, akisisitiza kuwa miradi hiyo ndiyo kielelezo cha ufanisi wa Serikali katika ngazi za chini. Amesema usimamizi makini, ufuatiliaji wa mara kwa mara na uwajibikaji ndiyo nguzo zitakazohakikisha wananchi wanapata matokeo halisi ya uwekezaji unaofanywa na Serikali.

Bw. Msovela pia ameipongeza Menejimenti ya Halmashauri inayoongozwa na Mkurugenzi Bi. Christina Bunini pamoja na Kamati ya CMT kwa hatua kubwa zilizopigwa katika kusimamia na kutekeleza miradi ya maendeleo tangu kuvunjwa kwa Baraza lililopita.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Mhe. Jamila Yusuph, amewataka waheshimiwa madiwani kusimamia kikamilifu mikopo ya asilimia 10, kuhamasisha suala la kilimo, na kuhakikisha ukusanyaji wa mapato unafanyika kwa ufanisi ili kuongeza mapato ya ndani ya Halmashauri.
Akizungumza mara baada ya kuthibitishwa, Mhe.Fimbo ameahidi kufanya kazi kwa karibu na madiwani wenzake ili kuleta maendeleo kupitia utekelezaji wa sera walizoahidi wakati wa kampeni za uchaguzi wa Oktoba mwaka huu.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved