Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imewajengea uwezo maafisa maendeleo ya jamii ili waendelee kuwa daraja muhimu la kuwasaidia vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu kuzipata fursa za zabuni zilizotengwa kwa ajili yao.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo yaliyotolewa na PPRA kwa maafisa maendeleo ya jamii na maafisa ununuzi wa halmashauri zote za Mkoa wa Katavi, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa huo, Bw. Florence Chrisant, amesema ni jukumu la watendaji hao kuwajengea uwezo wanufaika ili waweze kuingia kwenye ushindani wa zabuni zinazotolewa na serikali.
Bw. Chrisant amesema kuwa vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu wanapaswa kujengewa uwezo ili kunufaika na asilimia 30 ya bajeti ya tenda za Serikali, ambayo mwaka huu wametengewa bajeti ya zaidi ya Shilingi Trilioni Tano. Aidha, amewataka maafisa hao kutumia vyema elimu waliyopewa na PPRA kuhakikisha wanatoa elimu zaidi kuwaandaa na kuwawezesha wahusika ili waweze kuitumia fursa hiyo muhimu inayotolewa na serikali yenye lengo la kuwainua kiuchumi.
"Serikali imewekeza nguvu kubwa kuhakikisha makundi maalum yanashiriki kikamilifu kwenye zabuni za umma, na ninyi ndiyo daraja lao. Nataka muende mkatekeleze haya kwa vitendo, muwafikie walengwa katika maeneo yenu na kuhakikisha fursa hizi haziishii kwenye makaratasi bali zinawafikia wananchi kwa uhalisia.” Amesema Bw. Chrisant
Nao maafisa maendeleo ya jamii wakitoa shukrani zao, wamesema mafunzo hayo yamewaongeza uelewa mpana kuhusu taratibu za ununuzi wa umma na namna ya kuwafikia wanufaika kwa ufanisi. Wameahidi kuyatumia mafunzo hayo kwa vitendo kwa kuhakikisha wanawafikia vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu katika maeneo yote ya mkoa, kuwapa elimu sahihi kuhusu ushiriki wa zabuni pamoja na kuwawezesha kujiandaa kushindana katika tenda za serikali.
Aidha, wamesisitiza kuwa wataendelea kuwa daraja la taarifa, ushauri na uhamasishaji kwa makundi maalum ili kuhakikisha wanaendelea kunufaika na uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali katika kuboresha uchumi wa wananchi.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved