Pichani:Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe.Mwanamvua Mrindoko akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Majalila Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika alipofanya ziara katika Halmashauri hiyo 11 Agosti 2022
Baadhi ya Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Wilayani Mpanda Mkoani Katavi wameeleza mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe.Mwanamvua Mrindoko kuwa licha ya Serikali kufuta ushuru chini ya tani moja bado watoza ushuru ndani ya Halmashauri hiyo wameendelea kuwatoza wakulima wanaosafirisha mazao yao chini ya tani moja.
John Madege Mkazi wa Kijiji cha Majalila Wilayani Tanganyika ameeleza kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakisumbuliwa na kutozwa ushuru wa mazao yao chini tani moja licha ya makamu wa Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Philip Isdor Mpango kukekemea vikali tabia hiyo katika ziara yake Wilayani Tanganyika siku chache zilizopita.
Bw.Madege ameulalamikia utaratibu wa utoaji wa vibali vya kusafirisha ushuru chini ya tani moja katika ofisi za watendaji wa kata ndani ya Halmashauri hiyo kuwa ni changamoto kutokana na kukumbana na usumbufu Mkubwa.
Kufuatia changamoto hiyo Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe.Mwanamvua Mrindoko amewaelekeza Mkuu wa Wilaya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kuhakikisha kuwa wanakomesha tabia hiyo inayofaanywa na baadhi ya watumishi wasiokuwa waaminifu ambao wamekuwa wakikiuka maagizo na maelekezo ya viongozi wa ngazi za juu.
Amesema kuwa kitendo cha Wananchi kuendelea kutozwa ushuru chini ya tani moja ni kiashiria kuwa viongozi wa Halmashauri hiyo wameshindwa kusimamia kikamilifu maagizo ya viongozi wa ngazi za juu na kwamba wanapaswa kujitathmini.
Amewaelekeza Viongozi wa Halmashauri kuhakikisha kuwa Wananchi ambao wanasafirisha mazao chini ya tani moja wasitozwe ushuru kama ilivyoelekezwa na viongozi mbalimbali wa serikali na kwamba hatosita kuchukua hatua kwa kiongozi yeyote iwapo itathibitika kusababisha usumbufu huo kwa wananchi.
Kwa upande wake kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Bw.Desu Luziga ameeleza kuwa Halmashauri imetoa utaratibu wa kupata vibali kwa wakulima wanaosafirisha mazao chini ya tani moja lakini Wakulima wamekuwa na muitikio mdogo kukata vibali hivyo vinavyotolewa katika Ofisi ya Mtendaji wa Kata.
Ameongeza kuwa Halmashauri imekuwa ikipambana na baadhi ya wakulima wasio waaminifu wanaokwepa ushuru kwa kutumia mgongo wa wakulima wadogo wadogo ambapo wafanyabiashara wakubwa wamekuwa wakiwatumia wakulima wadogo na vijana wa bodaboda kusafirisha mazao chini ya tani moja ili kukwepa ushuru.
Bw.Luziga ameeleza kuwa pindi Watoza ushuru wanapobaini utoroshwaji wa mazao wa namna hiyo wamekuwa wakijizatiti kudhibiti hali hiyo ili kudhibiti mapato ya halmashauri ambapo amewataka wakulima wadogo wadogo kuhakikisha kuwa wanapata vibali vya kusafirisha mazao hayo katika ofisi za watendaji wa Kata ili kupuka usumbufu magetini.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved