Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika wamejitokeza kwa idadi kubwa katika kongamano maalum lililoandaliwa kwa ajili ya vijana, likiwa na lengo la kutoa elimu katika nyanja mbalimbali zikiwemo maandalizi ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru yatakayofanyika tarehe 23 Septemba, 2025.
Kongamano hilo, ambalo limefanyika katika Shule ya Sekondari Kabungu, limewapa vijana nafasi ya kuomba kuendelezwa kwa elimu ya ukombozi wa kifikra na kiuchumi ili iwe chachu ya kuinua maisha yao na kufikia maendeleo endelevu.
Vilevile, washiriki wamehimizwa kuepukana na matumizi ya dawa za kulevya, rushwa, pamoja na kuzingatia kinga dhidi ya UKIMWI na Malaria, kuimarisha lishe bora, kushiriki michezo kwa wingi na kulinda mila na desturi zao.
Mbali na hayo, vijana hao pia wamekumbushwa kushiriki kwa wingi katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru mnamo Septemba 23, 2025, ambapo miradi kadhaa ya maendeleo itapitiwa na kuzinduliwa rasmi.
Watoa mada ambao wamehudhuria na kushiriki katika kutoa elimu na hamasa kwenye kongamano hilo wamehusisha Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Bw. Oscar Mkende; Afisa Utamaduni, Remigius Bukhay; mwakilishi wa Dawati la Msaada wa Kisheria, Ramadhan Rashid; Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Kabungu, Bi. Ziada Mnayahe; Afisa Maendeleo ya Jamii, Weston Ndumbalu pamoja na Afisa Lishe, Anisa Kitera.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved