Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko, amesema kuwa mkoa huo umeanza kutekeleza utoaji wa huduma za Bima ya Afya kwa Wote, ambapo hatua iliyopo kwa sasa ni uhakiki na usaili wa kaya zisizojiweza.

Taarifa hiyo ameitoa leo, Februari 18, 2026, akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji na usimamizi wa miradi ya Serikali katika Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika ambapo amesema kuwa tayari utekelezaji wa Bima ya afya kwa wote umeanza katika hatua mbalimbali, na kwa sasa msisitizo uko kwenye uhakiki na utambuzi wa kaya zisizojiweza ili ziweze kuingizwa kwenye mpango huo.

"Katika Mkoa wa Katavi, kila halmashauri imejiwekea malengo ya kuzitambua kaya hizo, na zoezi hilo linaendelea katika Manispaa ya Mpanda pamoja na Halmashauri za Mlele pia leo Halmashauri ya Tanganyika imeanza rasmi zoezi hilo kwa kushirikiana na Mfuko wa Bima ya Afya pamoja na wadau wengine wanaohusika," amesema Mhe. Mrindoko.

Aidha amewataka viongozi na watendaji kuhakikisha wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa mpango huo, pamoja na kusimamia uandikishaji wa awali wa kaya zisizojiweza kupitia TASAF na ambazo hazipo katika mpango wa TASAF, lakini zinathibitika kuwa hazijiwezi, ziainishwe na kufanyiwa utaratibu unaostahili kisheria ili ziweze kujumuishwa na kupata huduma za Bima ya Afya kwa ufadhili wa Serikali.
Amesisitiza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wote, hususan wenye uhitaji maalum, wanapata huduma za afya kwa wakati bila kikwazo cha gharama.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved