Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, leo Febuari 11, 2025, amewasili mkoani Katavi kwa ziara ya kikazi inayolenga kujenga uwezo wa viongozi wa umma na wadau wa sekta ya sheria.

Mhe. Dkt. Homera amepokelewa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi na mwenyeji wake, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko, kabla ya kuanza rasmi ratiba ya mkutano wa kikazi unaohusisha mikoa ya Ukanda wa Magharibi na Nyanda za Juu Kusini.
Akiwa mkoani Katavi, atashiriki mkutano wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) pamoja na wajumbe wa Bodi za Wadhamini kutoka mikoa ya Katavi, Rukwa, Kigoma, Songwe, Mbeya na Tabora, wenye lengo la kuimarisha usimamizi na uwajibikaji wa bodi hizo.

Siku ya pili ya mkutano itawahusisha Maafisa Tarafa, Makatibu Tawala wa Wilaya na Wakuu wa Wilaya kwa lengo la kuwajengea uwezo katika kushughulikia masuala ya kisheria yanayowagusa wananchi, ikiwemo migogoro ya ardhi, ndoa na familia.

Mhe. Dkt. Homera amesema Wizara inaendelea kuboresha huduma za kisheria kwa kujenga na kukarabati mahakama za mwanzo ili kusogeza huduma karibu na wananchi.
“Serikali imejipanga kuhakikisha huduma za kisheria zinapatikana kwa urahisi na kwa kuzingatia misingi ya haki. Hatuwezi kufikia maendeleo bila kuimarisha uwajibikaji,” amesema.
Amesema wizara kwa kushirikiana na RITA imeweka utaratibu wa kutoa vyeti vya kuzaliwa ndani ya saa 48 baada ya kukamilika kwa usajili.
Aidha, Mhe. Dkt. Homera amepongeza uongozi wa Mkoa wa Katavi kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo, akieleza kuwa hatua hiyo imechangia kuimarika kwa huduma kwa wananchi na kuvutia uwekezaji.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko, amesema mkutano huo utawasaidia viongozi wa wilaya na tarafa kupata uelewa wa kina katika utatuzi wa migogoro inayowakabili wananchi.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Bw. Frank Kanyusi, amesema viongozi wa Wilaya ndiyo wanaokutana moja kwa moja na changamoto za wananchi, hivyo mafunzo hayo yataongeza ufanisi katika utoaji wa maamuzi kwa kuzingatia sheria.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved