Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko, leo Julai 28, 2025 amekutana na Mabaraza ya Wazee kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa Katavi kwa lengo la kuimarisha maandalizi ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Kikao hicho kimefanyika ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya Mkoa kuhakikisha uchaguzi unafanyika katika mazingira ya amani, mshikamano, na kuheshimu misingi ya haki, usawa na demokrasia. Wazee wamehusishwa kutokana na nafasi yao muhimu katika jamii kama wahifadhi wa mila, washauri wa kijamii, na daraja kati ya Serikali na wananchi.
Katika mkutano huo, Mkuu wa Mkoa amewashukuru Wazee kwa namna ambavyo wameendelea kuwa sehemu ya ustawi wa mkoa, hususan katika kushiriki kwenye masuala ya kijamii na kutoa ushauri kwa Serikali katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
Aidha, RC Mrindoko amewaomba Wazee kuendelea kuhubiri amani, mshikamano na upendo katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, huku akiwasihi kuwa mstari wa mbele katika kuzuia na kuripoti viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani vinavyoweza kujitokeza katika maeneo yao.
Pamoja na hilo, Mkuu wa Mkoa amewataka Wazee kuwa walimu kwa wagombea wa nafasi mbalimbali pamoja na wananchi, kwa kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa kushiriki uchaguzi kwa kufuata sheria, kuepuka rushwa, uchochezi, lugha za matusi, na vitendo vyote vinavyokinzana na maadili ya kitanzania.
Sambamba na hayo, Wazee wametoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi mahiri, utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya maendeleo, na dhamira yake ya kuimarisha ustawi wa wananchi kupitia sera na mipango ya kitaifa.
Mkutano huo umehitimishwa kwa wito wa Mkuu wa Mkoa kwa Wazee kushiriki kikamilifu katika zoezi la uchaguzi mkuu na kuendelea kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi hilo muhimu kwa mustakabali wa Taifa.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved