Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko, ameongoza hafla ya uzinduzi wa Juma la Elimu Kitaifa (GAWE 2025) kwa kutoa wito kwa wadau wa elimu kuendeleza ushirikiano na Serikali katika kuleta mabadiliko chanya kwenye sekta ya elimu nchini.
Katika hotuba yake, RC Mrindoko amesisitiza dhamira ya Serikali ya kuimarisha ushirikiano na Mtandao wa Elimu Tanzania kama sehemu ya juhudi za kuboresha ubora wa elimu, hususan kwa kuhakikisha elimu inakuwa jumuishi na yenye tija kwa kila mtoto wa Kitanzania.
Akiweka mkazo kwenye changamoto ya mimba na ndoa za utotoni maarufu kama “Chagulaga”, Mkuu wa Mkoa ameeleza kuwa mila na desturi zisizofaa zinaendelea kuwa kikwazo kwa elimu ya watoto wa kike. Amewataka wazazi na jamii kwa ujumla kulinda haki ya mtoto wa kike kupata elimu bila vikwazo vya kijamii na kiutamaduni.
Vilevile, amesisitiza umuhimu wa familia na jamii kuhifadhi mavuno kwa mwaka mzima ili kupunguza changamoto ya utoro mashuleni unaotokana na uhaba wa chakula, hali ambayo huathiri utekelezaji wa mpango wa lishe mashuleni na maendeleo ya kitaaluma ya wanafunzi.
Kwa upande wake, Afisa Elimu wa Mkoa wa Katavi, Bi. Dafroza Ndalichako, amewasilisha taarifa ya hali ya elimu mkoani humo, akieleza kuwa hadi kufikia Machi 31, 2025, jumla ya wanafunzi 29,782 wameandikishwa katika elimu ya awali, ikiwa ni asilimia 77.5 ya lengo la kuandikisha watoto 37,796.
Aidha ameendelea kuhimiza ushirikiano thabiti kati ya Serikali na wadau wa elimu katika kutatua changamoto hizo na kuimarisha maendeleo ya elimu mkoani Katavi.
Naye Mwenyekiti wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bi. Faraja Nyarandu, ameeleza kuwa mfumo wa elimu nchini unapaswa kujengwa kwa misingi ya utu, usawa na ubora. Amehimiza kuondolewa kwa adhabu zisizofaa mashuleni na matumizi ya mbinu mbadala za malezi zenye kujenga mazingira rafiki kwa watoto kujifunza.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa uwekezaji katika elimu ya ujuzi, lishe mashuleni, afya ya uzazi kwa vijana na miundombinu bora ili kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata elimu bora, salama na jumuishi.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved