Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko, ameziagiza Halmashauri zote za mkoa wa Katavi kuhakikisha zinapata mbegu bora za zao la ufuta na kuzisambaza kwa wakulima kwa wakati muafaka ili kuongeza uzalishaji msimu ujao. Amesema mbegu bora ni msingi wa kilimo chenye tija, na kuzitumia kunahakikisha wakulima wanapata mavuno mengi zaidi.
“Kwa kuwa masoko ya ufuta yameimarika kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani, fursa kwa wakulima ni kubwa zaidi kufanikisha uzalishaji bora na wenye tija. Halmashauri pia zitanufaika kwa mapato zaidi, ambayo yatawezesha kuendeleza huduma za kijamii na miundombinu,” amesema RC Mrindoko.
Pia, amewataka maafisa ugani kuwatembelea wakulima mara kwa mara na kuwapatia elimu ya mbinu bora za kilimo ili kuongeza uzalishaji na kuboresha tija. Amesisitiza kuwa elimu endelevu ni muhimu kwa wakulima kufanikisha kilimo cha kisasa.
RC Mrindoko ametoa kauli hiyo alipotembelea banda la Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika kwenye maonesho ya Nanenane 2025 yaliyohitimishwa leo katika Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya. Aidha, amepongeza mafanikio ya mkoa wa Katavi msimu huu na kusema maonesho ya mwaka huu yameonesha maendeleo makubwa ikilinganishwa na misimu iliyopita.
Vilevile, amewataka wakulima kujisajili ili kunufaika na mbolea za ruzuku zinazotolewa kwa gharama nafuu, hatua ambayo ni sehemu ya mkakati wa serikali kusaidia kupunguza gharama za uzalishaji.
“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kwa ajili ya malipo ya mbolea za ruzuku, hivyo wakulima wanatakiwa kunufaika kwa kujisajili mapema,” amesema RC Mrindoko.
Ameongeza kuwa ushirikiano wa karibu kati ya halmashauri, maafisa ugani na wakulima ni muhimu ili kuhakikisha mkulima yeyote anapata msaada unaohitajika kwa wakati unaofaa.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved