Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko, ameungana na mamia ya waumini na wakazi wa mkoa wa Katavi katika mazishi ya Askofu Dkt. Laban Ndimubenya, aliyekuwa kiongozi wa kiroho na mtetezi wa haki za jamii. Mazishi hayo yamefanyika katika Kanisa la New Harvest Church, Mikocheni, Manispaa ya Mpanda yakiambatana na majonzi makubwa kutoka kwa waombolezaji mbalimbali.
Katika hotuba yake, Mhe. Mrindoko ameeleza kuwa kifo cha Askofu Dkt. Laban ni pigo kubwa kwa Taifa, si kwa Kanisa pekee, kwani marehemu alikuwa mwalimu wa maadili mema, mshauri wa jamii, na kiongozi aliyekuwa mstari wa mbele katika kuleta maendeleo.
"Tumepoteza mtu wa pekee, mtu wa hekima na busara, aliyejitolea kwa dhati kuhudumia jamii kwa moyo wa upendo. Mchango wake haukuwa tu katika uwanja wa kiroho bali pia katika sekta za elimu, afya, na ustawi wa jamii. Alikuwa nguzo muhimu ya maendeleo katika mkoa huu wa Katavi na nchi kwa ujumla," amesema RC Mrindoko huku akitoa pole kwa familia, waumini, na wote walioguswa na msiba huo.
RC Mrindoko ameongeza kuwa Serikali itaendelea kumuenzi Askofu Dkt. Laban kwa kuthamini mchango wake na kuendeleza juhudi alizozianzisha katika sekta mbalimbali.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini, Mhe. Sebastian Kapufi, amemuelezea marehemu kama mtu aliyekuwa na maono makubwa kwa jamii na mwenye bidii isiyo na kifani katika kupigania maendeleo ya watu wake.
"Marehemu alikuwa kiongozi mwenye uthubutu, aliyeamini katika elimu na maendeleo ya jamii. Ameacha somo kubwa kwetu sote kwamba elimu haina mwisho na kwamba tunapaswa kuifuatilia kwa gharama yoyote ile ili kuleta mabadiliko chanya katika jamii zetu," amesema Mhe. Kapufi.
Mazishi hayo yamehudhuriwa na viongozi wa Serikali, maaskofu kutoka madhehebu mbalimbali ndani na nje ya nchi, pamoja na wananchi mbalimbaliwa mkoa wa Katavi.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved