Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mheshimiwa Mwanamvua Mrindoko, leo Januari 1, 2025, amesema kuwa wananchi wa Katavi wanapaswa kusherehekea mwaka mpya kwa amani na utulivu.
Katika salamu zake, Mheshimiwa Mrindoko ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jitihada kubwa zilizotekelezwa ndani ya mkoa wa Katavi mwaka 2024 na mipango kabambe iliyopangwa kwa mwaka 2025 na kuendelea.
Amesema kuwa mkoa umejipanga kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi, ikiwa ni pamoja na kuboresha sekta za elimu, maji, barabara, na afya. Lengo kuu ni kuhakikisha huduma hizi zinapatikana kwa ubora na kuwafaidisha wananchi wote wa Katavi.
Mheshimiwa Mrindoko ameweka msisitizo wa kuongeza uzalishaji katika sekta zote za uchumi, hasa kilimo, ambacho kimebainishwa kuwa uti wa mgongo wa usalama wa chakula. Ameeleza kuwa suala la usalama wa chakula ni ajenda muhimu kwa Tanzania na dunia nzima, na hivyo litapewa kipaumbele.
Amesema mkoa utaendelea kuimarisha masoko kwa mazao ya kilimo, mifugo, nyuki, na misitu, ikiwa ni pamoja na masoko ya minada na kuboresha Bandari ya Karema. Kwa mujibu wa Mheshimiwa Mrindoko, hatua hizi zinalenga kuwasaidia wakulima na wafanyabiashara wa mkoa wa Katavi kupata faida zaidi kutoka kwenye juhudi zao.
Katika sekta ya michezo na sanaa, Mkuu wa Mkoa amesema mkoa umeazimia kuibua vipaji vipya na kuendeleza sekta hiyo kwa kujenga miundombinu bora, ikiwa ni pamoja na kiwanja cha kisasa na timu ya mkoa itakayokuwa ikitangaza Katavi. Amesema juhudi hizi zinalenga kuimarisha maendeleo ya vijana na kutoa nafasi zaidi katika sekta ya burudani.
Aidha, Mheshimiwa Mrindoko amesema mkoa utaweka mkazo kwenye utunzaji wa mazingira, usafi, na upendezeshaji wa miji, akihimiza ushirikiano wa wananchi katika kuhakikisha Halmashauri zote za Katavi zinakuwa safi na zenye mvuto.
Ameeleza kuwa juhudi za kukuza utalii zitaharakishwa kwa kuhakikisha mbuga ya Katavi inatangazwa kikamilifu. Amesema mkoa umejipanga kuvutia wageni wa ndani na nje ya nchi ili kuchochea ukuaji wa uchumi katika sekta ya utalii.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved