Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko, amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote mkoani hapa kuepuka kuanzisha madeni mapya kwa wazabuni, kwa kuwa Serikali hutenga fedha kamili kwa ajili ya utekelezaji wa miradi na hulipa madeni yaliyopo kwa kutumia bajeti iliyopangwa bila kuongeza madeni mengine mapya.
Agizo hilo amelitoa leo, Mei 22, 2025, katika kikao kazi kilichowakutanisha Mkuu wa Mkoa, wazabuni na wakuu wa taasisi mbalimbali, ambapo walijadili jitihada zinazofanywa na Serikali kushughulikia madeni ya wazabuni pamoja na changamoto wanazokutana nazo.
Amesema kuwa baadhi ya watumishi wasio waaminifu wamekuwa wakichelewesha kushughulikia madai ya wazabuni, hali inayosababisha ongezeko la madeni. Ameelekeza kuwa wazabuni wanapaswa kuhakikisha wanazingatia matumizi sahihi ya nyaraka za zabuni ili kuepuka mkanganyiko unaoweza kujitokeza wakati wa ulipaji.
“Tuna mkakati wa kulipa madeni yote ya wazabuni kupitia bajeti ya kipindi cha miaka mitatu. Tayari tumeanza kupunguza madeni tangu bajeti ya mwaka 2024/2025, na tunatarajia hadi kufikia mwaka 2026/2027 tutakuwa tumemaliza kulipa madeni yote,” amesema Mhe. Mrindoko.
Ameongeza kuwa kutokana na jitihada hizo, Serikali ya Mkoa imefanikiwa kupunguza jumla ya madeni ya wazabuni kutoka shilingi bilioni 2.38 hadi kufikia malipo ya shilingi milioni 755.16 kwa baadhi ya wazabuni.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Mkoa wa Katavi, Bw. Amani Mahela, ametoa wito kwa wafanyabiashara kujiunga na chama chao ili kurahisisha ufuatiliaji wa madeni pamoja na upatikanaji wa taarifa sahihi kutoka kwa mamlaka husika.
“Taarifa nyingi kutoka serikalini huletwa katika ofisi zetu, lakini wafanyabiashara wengi hawazipati kwa sababu hatuna taarifa zao sahihi. Hivyo tunawasihi wajiunge na chama chetu ili tuweze kuwahudumia kwa ufanisi,” amesema Bw. Mahela.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved