Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko, leo Septemba 03, 2025 amefanya ziara ya kukagua hali ya utolewaji wa huduma ya maji katika Wilaya ya Mpanda, akisisitiza kuwa huduma ya maji safi na salama ni nguzo muhimu ya maisha ya wananchi, maendeleo ya kiuchumi, kijamii na hata usalama wa jamii.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, RC Mrindoko amesema lengo la ukaguzi huo ni kupata taswira ya utekelezaji wa miradi ya maji, pamoja na kujiridhisha kama wananchi wa mkoa huo wanapata huduma kwa kiwango kinachostahili.
Katika ukaguzi wake, RC Mrindoko ametembelea Mradi wa Maji wa Miji 28, ambao kwa sasa umekamilika kwa asilimia 51. Hata hivyo, ameeleza kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo na kutoa maagizo kwa Wizara ya Maji kupitia kwa Meneja wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mpanda kuhakikisha wanasimamia ipasavyo na kuharakisha ukamilishaji wake.
“Mradi huu ni tegemeo kubwa kwa wananchi wa Katavi. Kasi ya utekelezaji bado hairidhishi. Ni jukumu la Wizara ya Maji na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mpanda kuhakikisha maji yanaanza kutolewa mapema ili kuondoa changamoto ya mgao wa maji,” amesema
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa amekagua Mradi wa Urekebishaji na Maboresho ya Miundombinu ya Maji mjini, ambao tayari umeanza kutekelezwa. Hata hivyo, amebainisha kuwepo kwa changamoto za kifedha zinazokwamisha kasi ya ukamilishaji wake.
Amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji kuhakikisha fedha zinazohitajika, zaidi ya shilingi milioni 325, zinapatikana mapema. Kwa mujibu wa wataalamu walioko katika mradi huo, endapo fedha hizo zitapatikana haraka, ndani ya kipindi cha mwezi mmoja hadi mmoja na nusu mradi huo utaanza kutoa huduma na kupunguza kwa kiwango kikubwa mgao wa maji unaoathiri wananchi.
Aidha, RC Mrindoko ametoa agizo la siku 14 kwa Mamlaka ya Maji mjini Mpanda kuhakikisha wanakagua mtandao mzima wa mabomba ya maji katika mji, mitaa na vitongoji vyote. Amewataka kuhakikisha hakuna sehemu yenye uvujaji wa maji, mabomba yaliyopasuka, au upotevu wowote unaosababisha huduma isifikie walengwa.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved