Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko, ameihakikishia Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kuwa Mkoa wa Katavi haujawahi kuwa kikwazo katika utekelezaji wa shughuli yoyote iliyopangwa na Serikali, hivyo hata zoezi la uchaguzi mkoani humo linaendelea kuandaliwa kwa amani na utulivu.
RC Mrindoko ametoa kauli hiyo Aprili 29, 2025, wakati akiipokea na kuikaribisha Tume hiyo mkoani Katavi kwa ajili ya maandalizi ya zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Aidha, Mkuu wa Mkoa ameeleza kuwa tayari Serikali ya Mkoa imeanza kutekeleza jukumu hilo kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu uchaguzi na upigaji kura kupitia mikutano mbalimbali, na amewasihi wananchi kujitokeza kwa wingi katika vituo vitakavyotangazwa ili kusahihisha au kuhuisha taarifa zao.
“Tumejipanga kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani. Na kuanzia sasa, niseme tu kuwa ofisi yangu inatoa ushirikiano wa kutosha hadi pale uchaguzi utakapo kamilika,” amesisitiza Mheshimiwa Mrindoko.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama Kuu Asina Omari, amesema kuwa Tume imejipanga kikamilifu kwa ajili ya maandalizi ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, ikiwemo kwa Mkoa wa Katavi.
Amefafanua kuwa uboreshaji huo unahusisha kuwaandikisha raia wa Tanzania waliotimiza umri wa miaka 18 na zaidi, au watakaotimiza umri huo kabla ya tarehe ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, pamoja na wale ambao hawajapoteza sifa kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi au sheria nyingine yoyote.
Zoezi hilo pia linahusisha wapiga kura waliobadili makazi kutoka vituo walivyojiandikisha awali, waliopoteza sifa, wenye taarifa zisizo sahihi pamoja na waliopoteza au kuharibu kadi zao za kupigia kura.
Aidha, Mwenyekiti wa Tume hiyo amemuomba Mkuu wa Mkoa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha elimu kuhusu uboreshaji wa Daftari inawafikia wadau wote, akizingatia kuwa ana mtandao wa wasaidizi hadi katika ngazi za chini za utawala.
Zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa Mkoa wa Katavi linatarajiwa kuanza rasmi kuanzia Mei 1 hadi Mei 7, 2025.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved