Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe. Mwanamvua Mrindoko ametoa wito kwa wananchi wote wa mkoa wa Katavi kuendeleza mshikamano, amani na utulivu kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika tarehe 29 Oktoba 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 1, 2025, RC Mrindoko amesema Mkoa wa Katavi uko salama na wananchi wanaendelea na shughuli zao za kila siku bila hofu. Ameongeza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kikamilifu kuhakikisha kampeni na zoezi zima la uchaguzi linafanyika kwa hali ya usalama na amani.
“Tunapokaribia uchaguzi, nataka niwahakikishie wananchi wote wa Katavi kuwa hali ya usalama ni shwari. Vyombo vyetu vya dola vipo tayari kuhakikisha kila mkutano wa kampeni na kila hatua ya uchaguzi inafanyika kwa amani na utulivu,” amesema.
RC Mrindoko amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mikutano ya kampeni ya vyama mbalimbali, huku akisisitiza umuhimu wa kila mmoja kuepuka uvunjifu wa sheria na vitendo vinavyoashiria kuvunja amani. Amesisitiza kuwa jukumu la kutunza amani na mshikamano ni la wananchi wote kwa kushirikiana na Serikali.
Aidha, amewaomba viongozi wa vijiji, mitaa na kata kuhakikisha kuwa maeneo yao yanabaki salama na kutoa taarifa mapema kwa vyombo husika pindi viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani vinapojitokeza.
Pia amewataka wadau wote wa uchaguzi kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na mamlaka husika ili kuhakikisha haki na usawa vinazingatiwa kwa kila mshiriki wa uchaguzi.
“Nitoe rai kwa wananchi wote waliojiandikisha, kutunza vitambulisho vyao vya kupiga kura na kujitokeza kwa wingi ifikapo Oktoba 29, 2025 ili kutumia haki yao ya Kikatiba. Uchaguzi huu ni fursa muhimu ya kujenga mustakabali wa taifa letu,” aliongeza.
Mwisho amesisitiza kuwa Serikali imedhamiria kuona uchaguzi wa mwaka 2025 unafanyika katika mazingira ya utulivu, huku makundi yote ya kijamii ikiwemo vijana, wanawake, wazee, wanahabari, viongozi wa dini, vyama vya siasa na wadau wengine wakishiriki kikamilifu.
Kauli mbiu ya Uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 inasema "Kura yako, haki yako, jitokeze kupiga kura".
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved