Aprili 03, 2025.
Wataalamu wa Sekretarieti ya Mkoa na Halmashauri za Mkoa wa Katavi wamepatiwa mafunzo kuhusu uibuaji na utekelezaji wa miradi kwa mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko, amesema kuwa Mkoa wa Katavi una fursa nyingi za uwekezaji zinazoweza kutekelezwa kwa mfumo wa PPP. Amesisitiza kuwa kupitia mfumo huo, sekta binafsi inaweza kushirikiana na serikali kuwekeza katika miradi mbalimbali ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi.
Aidha, amebainisha kuwa Mkoa wa Katavi uko tayari kusimamia uibuaji na utekelezaji wa miradi ya PPP kwa kuhakikisha kuwa wananchi wenye sifa wanahamasishwa kushiriki kikamilifu. Amesisitiza dhamira ya mkoa katika kusaidia juhudi za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kufanikisha maendeleo ya kiuchumi kupitia miradi ya PPP.
Kwa upande wake, Dkt. Bravious Kahyoza ameeleza kuwa mfumo wa PPP ni nyenzo muhimu ya kuharakisha maendeleo kwa kushirikisha sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya umma. Amefafanua kuwa sekta binafsi inaweza kushiriki kwa njia mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu mipya na kuiendesha kwa niaba ya serikali, utoaji wa huduma kwa kutumia miundombinu iliyopo, na ukarabati pamoja na uendeshaji wa miundombinu ya serikali kupitia makubaliano maalum.
Akizungumzia faida za PPP, Dkt. Kahyoza ametaja kuwa mfumo huu huongeza ujuzi na ubunifu, hususan katika matumizi ya teknolojia, huimarisha ufanisi wa utoaji wa huduma, huongeza rasilimali fedha, na huchangia katika utunzaji bora wa mali za serikali.
Mafunzo haya yameleta mwanga kwa wataalamu wa Sekretarieti ya Mkoa na halmashauri za Mkoa wa Katavi juu ya fursa zilizopo kupitia mfumo wa PPP. Matarajio ni kuwa mafunzo haya yatawawezesha wataalamu hao kushiriki kikamilifu katika uibuaji wa miradi bora ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi wa Mkoa wa Katavi.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved