Serikali imetoa maelekezo kwa wakuu wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kuhakikisha kuwa ardhi haizuii wawekezaji vijana, pamoja na kuanzisha Benki ya Ardhi itakayowezesha vijana kukodishiwa ardhi kwa mikataba maalum kwa ajili ya uwekezaji wa kilimo.
Maelekezo hayo yametolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, kupitia taarifa iliyosomwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Beno Malisa, wakati wa ufunguzi wa maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya John Mwakangale, Jijini Mbeya, tarehe 2 Agosti 2025.
Taarifa hiyo imetoa maagizo kwa Wakuu wa Mikoa ya Katavi, Rukwa, Songwe, Ruvuma, Mbeya, Iringa, na Njombe, ikiwa ni pamoja na kuweka mkazo kwenye matumizi bora ya ardhi, matumizi sahihi ya viuatilifu na kemikali, usalama wa chakula katika ngazi ya kaya, kuepuka uvunaji wa mazao kabla ya wakati, na matumizi ya ardhi kwa ajili ya vijana wawekezaji.
Serikali imesisitiza kuwa kutokana na ongezeko la wawekezaji vijana, kuna haja ya kutenga ardhi kwa ajili yao ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za kilimo. Halmashauri zimetakiwa kutenga angalau hekta 100 kwa ajili ya vijana hao, kwa mikataba maalum, kama njia ya kuongeza mapato ya halmashauri na kuwezesha uwekezaji wa vijana kupitia benki ya ardhi.
Aidha, viongozi wa mikoa wameelekezwa kusimamia matumizi sahihi ya ardhi ili kuepusha migogoro kati ya wakulima na wafugaji pamoja na kuzuia uvamizi wa maeneo ya mapito ya wanyama pori kama tembo, hali ambayo imekuwa ikisababisha madhara kwa binadamu na mazingira.
Viongozi wa dini na kimila wameombwa kushirikiana na serikali katika kutoa elimu kuhusu usalama wa chakula kwa wananchi, kwa kusisitiza umuhimu wa kuhifadhi chakula kwa matumizi ya muda mrefu katika ngazi ya kaya, ili kupunguza athari za baa la njaa.
Viongozi wa mikoa wameelekezwa pia kusimamia kwa karibu uvunaji wa mazao ya biashara kama pareto, ili kuhakikisha kuwa yanavunwa kwa wakati unaofaa, hatua itakayosaidia kuongeza ubora wa mazao hayo na thamani katika soko la ndani na nje ya nchi.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved