Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Ndugu Ismail Alli Ussi ameongoza hafla ya ufunguzi wa mradi wa ujenzi wa nyumba za watumishi (2 kwa 1) katika Shule ya Sekondari Anna Lupembe, Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, mkoani Katavi, leo Alhamisi Septemba 25, 2025.
Mradi huo unaotekelezwa kupitia Programu ya Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) na umegharimu shilingi 1,110,000,000, fedha zinazotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kuboresha mazingira ya kufundishia na kufundishia.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji, Mwalimu Mkuu wa shule ameeleza kuwa ujenzi wa nyumba hizo umekamilika hatua inayotarajiwa kuongeza ari ya walimu, kuimarisha utendaji wa kazi na kupunguza changamoto za makazi kwa watumishi wa shule hiyo.
Akizungumza mara baada ya kukagua na kufungua mradi huo, Ndugu Ussi anatoa pongezi kwa Halmashauri ya Nsimbo, uongozi wa shule na wananchi kwa usimamizi makini na matumizi bora ya fedha za umma. Anasisitiza kuwa ubora wa ujenzi unathibitisha dhamira ya Serikali katika kuhakikisha walimu wanapata makazi salama na yenye hadhi, jambo linalochochea ari ya kutoa elimu bora.
“Mradi huu ni mfano wa uwajibikaji na matumizi sahihi ya rasilimali za Serikali. Nyumba hizi zinawapa walimu heshima na mazingira bora ya kuishi, jambo linaloongeza hamasa katika kazi yao ya malezi na ufundishaji,” amesema Ussi.
Katika hatua nyingine, Ndugu Ussi amezindua klabu mbalimbali shuleni hapo ikiwemo Klabu ya Lishe, Klabu ya Kupinga Rushwa na Klabu ya Kupamba na Rushwa, kama njia ya kuhamasisha maadili, afya na uwajibikaji miongoni mwa wanafunzi na jamii.
Aidha, kiongozi huyo ametoa vyeti vya pongezi kwa klabu hizo kama ishara ya kutambua mchango wao katika malezi ya kizazi chenye maadili bora. Sambamba na hatua hiyo, anagawa viti vitatu vya magurudumu kwa watu wenye ulemavu pamoja na vikinga jua kwa watu wenye ualbino katika Kata hiyo, hatua inayolenga kuimarisha usawa wa kijamii na kuwajengea mazingira salama ya maisha.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved