Katika kuadhimisha siku ya mtoto wa Afrika mkoani Katavi, Mkuu wa wilaya ya Mpanda Jamila Yusuph kwaniaba ya mkuu wa mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko amewaelekeza wakuu wa shule, maafisa elimu pamoja na wakuu wa idara za elimu katika mkoa huo kuhakikisha wanaweka sheria za shule ambazo zinatekelezeka ili kulinda usalama wa watoto wawapo shuleni.
Maagizo hayo ameyatoa leo Juni 16,2025 wakati wa sherehe za maadhimisho ya Mtoto wa Afrika kimkoa yaliyofanyika katika halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika ambapo amesema Serikali inalenga kumlinda mtoto dhidi ya ukatili.
"Kusimamia maadili na nidhamu itasaidia watoto kuzingatia masomo na kuwaepusha kutumia muda mwingi kufanya matendo vya uovu na pia wazazi endeleeni kuhakikisha ulinzi wa watoto ikiwemo kuwasimamia katika matumizi ya simu, muwaepushe na mitandao ya kijamii," Amesema Mhe. Jamila.
Akisoma Risala ya baraza la watoto Mkoa wa Katavi Maria Samike amesema zipo changamoto mbalimbali katika jamii ambazo zimefanya watoto washindwe kupata haki za msingi pamoja na kuzifikia ndoto zao.
Miongoni mwa changamoto hizo ameziainisha kuwa ni uelewa mdogo wa jamii juu ya umuhimu wa elimu, umaskini, migogoro ya ndoa inayosababisha wazazi kutengana, mimba za utotoni na ukatili wa kijinsia hasa (vipigo, ubakaji, ulawiti).
"Bado jamii zetu zinaendeleza mila zenye kuleta Madhara, imani za kishirikina na mila potofu ikiwemo chagulaga kwa wasichana ambayo imekuwa ikikatisha ndoto za wasichana wengi," Amesema Maria.
Kwa upande mkuu wa wilaya ya Tanganyika Onesmo Busweru amesema serikali imewekeza katika kuwajenga walimu na walezi katika kuhakikisha watoto wanakuwa salama. Na amewataka watoto kuitunza na kuitetea serikali na kuwa wazalendo wasichochewe katika kuleta vurugu watakapokuwa wakubwa.
Maadhimisho siku ya mtoto wa Afrika 2025 yanabebwa na kauli mbiu isemayo Mtoto:Tulipotoka, Tulipo na Tuendako.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved