Na:OMM- Katavi
Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe.Mwanamvua Hoza Mrindoko ametoa siku 7 kwa Halmashauri zote Mkoani humo kuhakikisha Fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa Afua za Lishe zinatumika kama ilivyokusudiwa.
Mhe.Mrindoko ametoa agizo hilo Februari 1, 2022 katika kikao cha Tathmini ya Lishe kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Mpanda kilichokutanisha Wadau mbalimbali wa lishe Mkoani humo.
“Tumegundua kuwa Halmashauri zetu zote bado hazijaweza kutoa kwa kiasi kile kilichopangwa Fedha za mapato ya ndani ambazo zimekusudiwa na zimeelekezwa kwenda kufanya kazi katika Afua za Lishe na hilo linatokana na uzembe wa kusimamia vizuri, hivyo tumeelekeza ndani ya siku 7 Halmashauri zote zikahakikishe Fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya afua za Lishe zinatumika kama ilivyokusudiwa.”Alisema Mkuu wa Mkoa Mrindoko.
Aidha Mkuu wa Mkoa Mrindoko amewaagiza Wakurugenzi na Waganga wakuu wa Halmashauri Mkoani humo kutoa maelezo kwa Maandishi kwa nini wasichukuliwe hatua za kinidhamu kwa kushindwa kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Bajeti ya Afua za Lishe kwa kipindi cha miezi 6 kuanzia Julai 2022 hadi Disemba 2022.
Katika hatua nyingine Mhe.Mrindoko amewaelekeza Wataalamu wa Afya akuandaa vipeperushi vitakavyoainisha makundi mbalimbali ya chakula kulingana na mazao yanayolimwa ndani ya Mkoa wa Katavi na kusambaza kipeperushi hicho kwa Wananchi ili kujenga uelewa wa namna ya Ulaji kwa kuzingatia Lishe Bora kusudi kuondokana na changamoto ya udumavu na ukondefu.
Kwa Upande wake Afisa Lishe Mkoa wa Katavi Bi.Asnati Mrema amesema wataalamu wa Mkoa wamepokea wamejipanga kutekeleza kikamilifu maagizo yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa.
“Tulikuwa tunafanya tathmini ya mkataba wa Lishe kwa Miezi 6 ambapo tumepitia tumepitia mkataba na kuona utekelezaji wa viashiria vyote ndani ya Mkataba lakini katika kiashiria cha Fedha ndio kiashiria ambacho kama Mkoa hatukufanya vizuri ambapo Mkuu wa Mkoa ameagiza kiashiria cha Fedha kifanyiwe maboresho”Alisema Bi.Asnath Mrema.
Ameeleza kuwa Mkoa wa Katavi unazalisha kwa wingi lakini una changamoto ya udumavu kwa Asilimia 33, Tumejipanga kuhakikisha kuwa Elimu ya Lishe kwa Wananchi inatolewa kikamilifu kwa Wananchi kuzingatia muongozo ulitolewa na Wizara ya Afya ambapo mikutano ya hadhara,vyombo vya habari na njia nyinginezo zitatumika katika kuhakikisha Elimu ya Lishe inawafikia Wananchi.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved