Kilimo si tu kazi ya mikono, bali ni sayansi, biashara, na chanzo kikuu cha maendeleo kwa jamii nyingi nchini. Katika mazingira ya sasa ya mabadiliko ya tabianchi na mahitaji makubwa ya chakula bora, nguvu mpya katika sekta ya kilimo ni jambo lisilokwepeka. Maonesho ya Nanenane yanakuja kama jukwaa la kuhamasisha mabadiliko hayo kwa vitendo kupitia elimu, teknolojia, na ubunifu wa wadau wa ndani na nje ya sekta.
Mkoa wa Katavi, ukiwa miongoni mwa washiriki wa maonesho haya, umejipanga kwa namna ya kipekee. Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Katavi anayesimamia Uchumi na Uzalishaji, Bw. Nehemia James, amesema kuwa maandalizi yamekamilika kwa asilimia mia moja. Halmashauri zote tano, Tanganyika, Mpimbwe, Nsimbo, Mlele na Manispaa ya Mpanda, zimeshawasili jijini Mbeya na zimepanga kuonesha ubunifu wa wakulima, wafugaji na wavuvi wa Katavi kwa mwaka huu.
Bw. Nehemia ameweka wazi kuwa kila banda la Katavi litakuwa darasa wazi kwa wananchi. Kutakuwa na maafisa ugani waliobobea, vipando bora, mifano halisi ya kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi, pamoja na bidhaa za wajasiriamali wa Katavi zilizoongezewa thamani kama vile asali safi, mbegu bora, na bidhaa za biashara ya kaboni. Wananchi wanatarajiwa kunufaika kwa kupata maarifa ya moja kwa moja yatakayowawezesha kubadilisha mbinu zao za uzalishaji.
Maonesho ya Nanenane kwa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yatafunguliwa rasmi tarehe 2 Agosti, 2025 katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, atakuwa mgeni rasmi katika ufunguzi huo, ambao unatarajiwa kuvuta maelfu ya washiriki na wageni kutoka mikoa yote ya Nyanda za Juu Kusini.
Kauli mbiu ya mwaka huu: "Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025." Ni wito kwa Watanzania kutambua nafasi ya uongozi makini katika kusukuma mbele sekta zinazowagusa moja kwa moja katika maisha ya kila siku.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved