Sekta ya afya Mkoa wa Katavi imeanza hatua za awali za kutekeleza mkakati wa kukabiliana na magonjwa mapya ya mlipuko na yanayojirudia rudia kwa kuyatambua maeneo hatarishi yanayochochea kuendelea kuwepo kwa magonjwa hayo.
Utelekezaji wa mikakati hiyo umetangazwa rasmi na Mganga mkuu wa Mkoa wa Katavi Dkt Jonathan Budenu katika kikao cha tathimini ya huduma za usafi wa afya mazingira pamoja na huduma za maji safi na vyoo vijijini kilichofanyika leo Julai 22,2025, ambapo amesema lengo ni kufikia makubaliano ya kile kinachoenda kufanyika katika jamii ili iweze kupata uelewa kuhusu afya mazingira.
“Tukiyatambua maeneo yote ambayo ni hatarishi kwa magonjwa ya mlipuko, itasaidia kuweka mkakati wa pamoja wa kukabiliana na magonjwa hayo lakini pia kila mmoja aliyetoka katika halmashauri akafanye upembuzi ili kubainimaeneo hayo na tuweze kuwa na mkakati wa pamoja ili kuhakikisha tunafikia malengo ya kila mtanzania kuwa anapata huduma bora za afya,” amesema Dkt Budenu.
Akizungumza na waganga wakuu wa Halmashauri pamoja na maafisa afya katibu tawala Mkoa wa Katavi, Albert Msovela amewataka kuendelea kuchukua tahadhari na kujikinga dhidi ya magonjwa ya mlipuko kwa kujenga uelewa mpana wa matumizi ya vyoo bora katika jamii.
“Hali ya uwepo wa vyoo bora bado hairidhishi, kwa mwananchi wa kawaida anaweza kuona ni hali ya kawaida lakini ukiwaza kwanini tunakuwa na mlipuko wa magonjwa ni kwa sababu hatuna matumizi sahihi ya vyoo ambavyo vipo, Madhara yake tumeyaona kutokana hali ya magonjwa ya mlipuko inavyokuwa kwenye jamii,” amesema Msovela.
Akizungumza kwaniaba ya washiri wa kikao hicho Dkt. Alex Mrema, ameahidi kwenda kuyafanyia kazi yale yote yaliyoelekezwa ili kufikia malengo ya serikali ya kuhakikisha wanaweka mikakati thabiti ya kutokomeza magonjwa ya mlipuko.
Takwimu za uwepo wa vyoo bora ngazi ya kaya zinaainisha kuwa mkoa wa Katavi unajumla ya 66.3% ya vyoo bora sawa na idadi ya kaya 129,646 idadi ya kaya zinazotumia vitakasa mikono ni 48.43% na kaya ambazo hazina vyoo ni asilimia 0.1% pekee.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved