Pichani:Mganga Mkuu wa Mkoa wa Katavi Dkt.Omari Sukari akishiriki kutoa Matone ya Chanjo ya POLIO kwa watoto chini ya miaka 5 katika Kituo cha Afya Ilembo Manispaa ya Mpanda alipozindua Kampeni hiyo ya Kitaifa Kimkoa 18 Mei 2022.
Na: John Mganga-IO Katavi RS
Kampeni ya Utoaji wa Chanjo ya Matone ya POLIO Kwa watoto wenye umri chini ya miaka 5 imezinduliwa rasmi Mkoani Katavi ikiwa ni utekelezaji wa Ratiba ya Kampeni ya Zoezi hilo Kitaifa
Katika Mkoa wa Katavi Kampeni hiyo inatekelezwa katika Wilaya za Mpanda,Mlele,Mpimbwe na Tanganyika ambapo uratibu wa Utoaji wa Matone ya Chanjo ya POLIO umeanza kutekelezwa katika ngazi za Halmashauri zote ndani ya ilaya hizo.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Katavi amezindua Kampeni hiyo kwa kushiriki kutoa chanjo ya Matone ya POLIO ambapo pia amepita baadhi ya nyumba na kutoa chanjo kwa watoto chini ya miaka 5 walioko majumbani katika baadhi ya Nyumba katika Kata ya Ilembo.
Akizungumza wakati wa Uzinduzi wa Kampeni hiyo katika Kituo cha Afya Ilembo kilichopo Manispaa ya Mpanda, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Katavi Dkt.Omari Sukari ametoa rai kwa Wazazi,Walezi na Wananchi kwa Ujumla kutoa Ushirikiano kwa Timu za Wataalamu zinazopita nyumba kwa nyumba kutoa huduma hiyo ya Matone ya Chanjo ya POLIO.
Amesema lengo la Mkoa ni kuhakikisha kuwa watoto wote wenye Umri chini ya Miaka 5 wanafikiwa na huduma hiyo na kwamba wamejipanga kuhakikisha kuwa maeneo yote yenye watoto kama vile Mashuleni,pamoja na vituo vya Malezi yanafikiwa.
Mganga Mkuu wa Mkoa ametoa wito kwa Wananchi kupuuza Taarifa zote za Upotoshwaji zinazotolewa na watu wasio na nia njema na badala yake waelekeze maswali ya Ufahamu kwa wataalamu wa Afya wanaopita katika maeneo mbalimbali ili kutoa huduma ya Chanjo hiyo.
Kwa Upande wao Wazazi na walezi waliojitokeza katika kituo cha Afya Ilembo waliowaleta watoto wao wameishikuru Serikali kwa namna ambavyo imechukua hatua za Haraka za kuwakinga watoto na hatari ya Ugonjwa wa POLIO.
Mnamo 13 Mei 2022,Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe.Mwanamvua Mrindoko katika mkutano na Vyombo vya Habari alisema ni muhimu kwa Wananchi kwa Wananchi kutoa Ushirikiano katika kufanikisha utekelzaji wa Kampeni ya utoaji wa Chanjo ya Matone ya POLIO kwa watoto wote wenye umri chini ya miaka 5 ili kufikia azma ya Mkoa ya kuwachanja watoto 189,465.
Kampeni ya Utoaji wa Chanjo ya Matone ya POLIO kwa watoto wenye Umri chini ya miaka 05 itadumu kwa muda wa siku nne baada ya kuanza 18 Mei 2022 ambapo inatarajia kumalizika ifikapo 21 Mei 2022.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved