Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda imeibuka nafasi ya tatu kati ya halmashauri zilizofanya vizuri katika maonesho ya kilimo, mifugo na uvuvi ya Nanenane 2025 Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, yaliyohitimishwa leo katika viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.
Tuzo ya ushindi imepokelewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, Bi. Sophia Kumbuli ambaye amekabidhiwa na Mgeni Rasmi wa hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhe. Charles Makongoro Nyerere, mbele ya umati wa washiriki na wageni waalikwa.
Katika matokeo ya mwaka huu, Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa imeibuka kinara kwa nafasi ya kwanza, ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Iringa katika nafasi ya pili. Ushindi wa Mpanda unatajwa kuwa umetokana na maandalizi thabiti, mshikamano wa wataalamu wake na ubunifu wa kuonesha teknolojia rafiki na zenye tija kwa sekta ya kilimo na mifugo.
Maonesho ya mwaka huu yamebeba kaulimbiu isemayo: “Chagua viongozi bora kwa maendeleo endelevu ya kilimo, mifugo na uvuvi.” Kaulimbiu hii imetoa ujumbe mahsusi kwa wadau wote wa sekta hizi muhimu, ikiwataka kuweka kipaumbele kwa uongozi wenye dira na maono ya maendeleo.
Kupitia ushindi huu, Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda imeonesha dhamira yake ya kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kukuza sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi, na kutoa mchango wa moja kwa moja katika maendeleo ya wananchi wake na taifa kwa ujumla.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved