Benki ya CRDB Mkoa wa Katavi imetoa madawati 60 kwa Shule ya Sekondari ya Wasichana Katavi, iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, ikiwa ni sehemu ya mpango wa benki hiyo wa kurudisha fadhila kwa wananchi kupitia faida iliyopatikana.
Akikabidhi madawati hayo, Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Bi Jennifer Tondi, ameeleza kuwa Benki ya CRDB kupitia mkakati wake wa Keti Jifunze itaendelea kushirikiana na serikali katika kuchangia huduma mbalimbali za kijamii mkoani Katavi.
Amesema kuwa pamoja na majukumu yake ya kibenki, benki hiyo imetenga asilimia moja ya faida yake ili kuhudumia mahitaji ya jamii katika sekta mbalimbali, ikiwemo elimu.
Aidha, ameeleza kuwa lengo ni kuhakikisha tatizo la wanafunzi kuketi chini linaondolewa kabisa kupitia kampeni ya Keti Jifunze, na kwamba benki itaendelea kushughulikia changamoto ya upungufu wa madawati mashuleni kadri faida itakavyopatikana.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Mhe. Jamila Yusuph, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi, ameishukuru Benki ya CRDB kwa mchango wake katika maendeleo ya wilaya hiyo, amewataka wadau wengine kuendelea kujitokeza kuchangia maendeleo, na amewasisitiza wanafunzi kusoma kwa bidii pamoja na kuyatunza madawati hayo ili yaweze kusaidia vizazi vijavyo.
Aidha, ametoa wito kwa wanafunzi hao kuepuka mahusiano ya kimapenzi katika kipindi cha masomo yao, akisisitiza kuwa kufanya hivyo kutawawezesha kuzingatia elimu na kujiepusha na changamoto zinazoweza kuhatarisha maisha yao ya baadaye.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved