722 Wafanyiwa Ukatili Katavi.
Jamii Katavi yahimizwa kukemea,kukomesha Vitendo vya Ukatili.
Jumla ya watu 722 wameripotiwa kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia ambapo ndani ya saa 72 kesi 63 za ukatili wa kijinsia ziliripotiwa kwa kipindi cha Mwaka 2021 Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Katavi Bi Anna Shumbi ameeleza.
Akitoa hotuba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe Mwanamvua Mrindoko mbele ya wakazi wa Mtaa wa Rungwa katika uzinduzi wa kampeni ya Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia 25 Novemba 2022, Afisa maendeleo ya Jamii mkoa ameeleza kuwa matukio ya ukatili wa Kijinsia yaliyoongoza zaidi ni ukatili wa kisaikolojia na lugha ya matusi ambao ulikuwa ni kesi 396,ukatili wa kimwili hasa kipigo kesi 248 na ukatili wa kingono kesi 78 kwa mwaka 2021.
Ameeleza kuwa chanzo cha ukatili wa kijinsia hususani kwa watoto ni Familia huku maeneo mengine ambako ukatili hufanyika kwa kiasi kikubwa kuwa ni Migodini Masokoni na kwingineko hivyo ni muhimu Jamii kuchukua hatua za makusudi kupunguza na kuondoa kabisa matukio ya vitendo vya ukatili unaofanywa kwa Watoto na Wanawake.
Ametadharisha Wananchi kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya usafi wa mazingira haswa katika kipindi cha masika ili kuondoa mazingira ya vichaka yanayoweza kushawishi wasio na nia njema kufanya vitendo vya Ukatili kwa Wanawake na watoto pamoja na kuepuka kuwatuma watoto nyakati za Jinoni.
Kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Mpanda Sophia Kumbuli amesema ni muhimu Jamii kuelekeza nguvu katika mapambano ya ukatili wa Kijinsia kwa watoto wa kiume pia badala ya wa kike na wanawake peke yake kwa kuwa watoto wa kiume nao wamekuwa wahanga wakubwa wa vitendo vya ukatili ambapo baadhi wamekuwa wakifanyiwa vitendo visivyofaa ikiwemo kulawitiwa na mengine mengi.
Maadhimisho hayo ya kupinga ukatili wa kijinsia kwa watoto na Wanawake yaliyozinduliwa 25 Novemba 2022 yanayoadhimishwa na Serikali kwa kushirikiana na Asasi mbalimbali zisizo za kiserikali yatadumu kwa siku 16 ambapo kilele chake kitakua 10 Desemba, 2022 yakibebwa na kaulimbiu inayosema Kila uhai una thamani tokomeza mauaji na ukatili kwa Wanawake Watoto.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved