Wakati waumini wa dini za Kikristo na Kiislamu wakiingia katika kipindi cha mfungo wa Kwaresma na Ramadhani, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko, amewataka wafanyabiashara kuhakikisha hawapandishi bei za bidhaa, akisisitiza kuwa mkoa wa Katavi una chakula cha kutosha na bidhaa zinapatikana kwa urahisi.

Akizungumza leo, Februari 19, 2025 wakati wa mkutano wake na wafanyabiashara wa Soko Kuu la Manispaa ya Mpanda, RC Mrindoko amesema lengo la kufika sokoni hapo ni kusikiliza kero na changamoto wanazopitia wafanyabiashara pamoja na kufuatilia mwenendo wa bei za bidhaa baada ya kuanza kwa mfungo wa Kwaresma na Ramadhani.

“Nasisitiza wafanyabiashara muendelee na bei zilezile za awali. Mkoa wa Katavi hauna njaa, chakula kipo cha kutosha na hakuna sababu ya kupandisha bei,” amesema RC Mrindoko.
Akiongeza kuwa Serikali haitavumilia upandishaji holela wa bei, huku akiwataka wananchi kutoa taarifa mara moja endapo watakutana na ongezeko la ghafla la bei sokoni.

“Mteja akiona bei imepanda bila sababu, atoe taarifa mara moja kwa mamlaka husika ili hatua zichukuliwe,” amesisitiza.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa amemuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda kuhakikisha kuwa ifikapo Machi 19, 2026, soko hilo linakuwa limefanyiwa ukarabati, akieleza kuwa msimu wa mvua umebainisha changamoto ya mapaa yanayovuja na kuathiri shughuli za biashara.

RC Mrindoko ametumia fursa hiyo kuwatakia waumini wote wa dini za Kikristo na Kiislamu mfungo mwema wa Kwaresma na Ramadhani, akiwataka kuendelea kudumisha amani, mshikamano na upendo katika kipindi chote cha ibada.


Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved