HUDUMA YA KUCHUJA DAMU (DIALYSIS): TUMAINI JIPYA KWA WAGONJWA WA FIGO KATAVI
Na Samirah Yusuph, Katavi-RS
“Kusingekuwa na hizi mashine nisingekuwa hai, kwa sababu ningepata wapi huduma? Ninaishukuru serikali kwa kuleta huduma hii na kuisogeza hadi katika mikoa ya pembezoni, Awali ilibidi kusafiri hadi Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya, jambo lililokuwa na gharama kubwa kwani ililazimu mtu kuhama kabisa nyumbani ili awe karibu na huduma,” anasema mmoja wa wanufaika, anayepata matibabu ya kuchuja damu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi.
Mnufaika huyo alikuwa ameunganishwa kwenye mashine ya kusafisha damu kupitia mirija maalum wakati akizungumza, Akiwa ni miongoni mwa wagonjwa watano waliokuwa wakipata huduma hiyo ndani ya jengo jipya lililogharimu zaidi ya shilingi milioni 275, Jengo hilo ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma za kuchuja damu kwenye hospitali za rufaa za mikoa.
Mnufaika mwingine alieleza kuwa ilimlazimu kuhama kutoka katika mkoa aliokuwa akiishi hapo awali kwenda mkoani Mbeya ili kupata huduma katika hospitali ya rufaa kanda ya Mbeya jambo ambalo lilimtenga na familia kwa kipindi cha miaka miwili.
Picha; Mmoja wa wanufaika wa huduma ya kuchuja damu inayopatikana katika hospital ya Rufaa Mkoa wa Katavi akiendelea na matibabu.
“Tulikuwa tunahangaika sana kwenda Mbeya au Dodoma, nililazimika kuhamia Mbeya tangu mwaka 2022 ili nipate matibabu, Nimerudi baada ya kuwa na uhakika wa kupata huduma hapa Katavi. Nashukuru sana kwa hili, kwani mateso tuliyopitia hayakuwa madogo,”
Serikali imelenga kupunguza gharama na usumbufu wa safari kwa wagonjwa wa figo, kwa kusambaza zaidi ya mashine 137 za kuchuja damu katika hospitali 15 za rufaa nchini, na jumla ya vituo 73 vilivyo idhinishwa kutoa huduma ya kuchuja damu, Hatua hii inalenga pia kuimarisha huduma za tiba kwa magonjwa sugu yasiyoambukiza (NCDs) na kuongeza ushindani katika soko la huduma za afya.
“Miaka kumi iliyopita, tulimpoteza Mzee wetu kwa ugonjwa wa figo sababu hatukuweza kumudu gharama za matibabu, Kipato chetu hakikuweza kumudu gharama za matibabu, zamani ukisikia mtu anaumwa figo, ilikuwa sawa na kutangaza kifo hakukuwa na tiba ya haraka kama sasa,” anasema Lilian Mwaikambo, ambaye kwa sasa anamuuguza mjomba wake katika Hospitali ya Rufaa ya Katavi.
Picha; Miongoni mwa wanufaika wa huduma ya kuchuja damu inayopatikana katika hospital ya Rufaa Mkoa wa Katavi akiendelea na matibabu.
Kuchuja damu ni matibabu maalumu yanayofanyika pale ambapo figo za mtu zimeshindwa kufanya kazi yake ipasavyo, hasa kazi ya kuchuja sumu na taka mwilini, pamoja na kusawazisha maji, chumvi, na madini muhimu mwilini kama vile potasiamu na sodiamu.
Kuna aina mbili za Dialysis ambazo Hemodialysis (HD) ambapo damu ya mgonjwa hutolewa kupitia mrija maalum (katheta) na kupelekwa kwenye mashine ya dialysis, Mashine hiyo huchuja damu na kuirudisha mwilini ikiwa safi na hufanyika mara 2 hadi 3 kwa wiki, kila kikao huchukua zoezi huchukua masaa matatu hadi matano.
Aina nyingine ni Peritoneal Dialysis (PD), hapa hakuna mashine badala yake maji maalum (dialysate) huingizwa tumboni kwenye utando wa ndani wa tumbo (peritoneum) ambapo taka hutolewa kupitia mfumo huo kwa kutumia shinikizo la kimazingira.
Picha; Muonekano wa baadhi ya mashine zinazopatikana katika jengo la kuchuja damu katika hospitali ya Rufaa Mkoa wa Katavi.
“Magonjwa yasiyoambukiza yanaongezeka katika jamii, ninaishukuru serikali kwa kusogeza huduma hizi muhimu karibu na wananchi hivyo itaimarisha elimu ya afya ya jamii hali itakayoisaidia jamii kuepuka magonjwa yasiyo ya kuambukiza , lakini inaposhindikana, tiba inakuwa ipo karibu,” anasema Neema Mwamwaja, mkazi wa Mpanda.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi, Dkt. Frank Elisha, anasema tangu jengo la dialysis likamilike Februari 2025 hadi Juni 2025, jumla ya huduma 195 za usafishaji damu zilitolewa bila kuripotiwa kifo chochote.
“Huduma zinatolewa kwa asilimia 100 hivyo ninatoa wito kwa wananchi kuendelea kuzingatia mtindo bora wa maisha ili kuepuka magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza,”
alisema Dkt. Elisha.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linachukulia magonjwa yasiyoambukiza kama tishio kubwa la afya duniani, likitoa mkazo madhubuti kwenye ugonjwa wa figo hasa pale figo zinapofeli kufanya kazi Mei 2025, WHO ilipitisha azimio la kwanza la afya ya figo kwenye mkutano wake wa World Health Assembly, likitambua ugonjwa wa figo kufeli kama changamoto kubwa ya afya ya umma na dunia nzima .
Lengo likiwa ni kuhakikisha ugonjwa wa figo unaunganishwa na mikakati ya magonjwa yasiyoambukiza, pamoja na kuanzishwa mipango ya utambuzi mapema, huduma ya msingi, na usawa wa matibabu ya kusafisha damu (Dialysis) .
Picha; Muonekano wa nje wa Jengo la Kuchuja damu katika hospitali ya Rufaa Mkoa wa Katavi(picha ilipigwa wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko alipotembelea jengo hilo.)
Mpango mkakati wa sekta ya afya (HSSP V) wa sera ya afya unalenga kupunguza vifo na magonjwa yasiyoambukiza kwa kutumia mbinu za kuzuia, utambuzi wa mapema, matibabu na msaada wa kitaalamu kwa mtu aliyepoteza uwezo wa mwili ua kiakili ili aweze kujitegemea tena (Rehabilitation)
Mpango mkakati huo unaeleza kuwa magonjwa yasiyo ambukiza yanachangia 30% ya vifo nchini kutokana na mtindo usiofaa wa maisha, lishe isiyofaa, na uchafuzi wa mazingira, serikali inaendelea kuboresha utoaji wa Huduma za magonjwa sugu na yasiyoambukiza kama kisukari, presha na magonjwa ya moyo ikiwa ni pamoja na kutafiti na kudhibiti changamoto za magonjwa ya figo.
Sera inaweka mkazo katika kuwajengea uwezo na mafunzo, namna ya utambuzi na usimamizi wa magonjwa sugu na yasiyo ya kuambukiza, ikiwemo utunzaji wa figo na matibabu ya matatizo yanayotokana na kisukari na presha, Maboresho ya Miundombinu na vifaa pamoja na Ushirikishaji na Jamii.
Kwa kipindi cha miaka mitano, sekta ya afya mkoani Katavi imepokea jumla ya shilingi bilioni 41.015 kwa ajili ya uboreshaji wa huduma za afya, fedha hizo zimetumika kujenga hospitali ya rufaa ya mkoa, hospitali nne za wilaya, vituo vya afya 11, zahanati 47, na ukarabati wa hospitali moja ya zamani, baadhi ya vituo vya afya pamoja na vifaa na vifaa tiba.
Akieleza mafanikio ya uwepo wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi, Mkuu wa Mkoa huo Mwanamvua Mrindoko alisema kwa sasa haititaji kuwasafirisha wagonjwa kwenda mbali kwa ajili ya huduma za kibingwa kama upasuaji, mifupa, magonjwa ya ndani, masikio, pua na koo pamoja na kuchuja damu.
“Upatikanaji wa huduma za afya za kibingwa umeimarika, serikali imeboresha miundominu ya afya ili kuondoa usumbufu kwa wananchi wa kufuata huduma za afya mbali pamoja na kupata huduma za uchunguzi wa magonjwa mbalimbali,” alisema Mhe. Mrindoko.
Hadi Juni 2025, Mkoa wa Katavi una jumla ya vituo 161 vinavyotoa huduma za afya. Kati ya hivyo, kuna Hospitali 1 ya Rufaa ya Mkoa, Hospitali 5 za Halmashauri, Vituo vya Afya 28, na Zahanati 127.
Kuimarika kwa huduma afya za kibingwa katika ngazi ya Mkoa na huduma za afya katika ngazi za msingi ikichangizwa na upatikanaji wa huduma bora za afya katika vituo vya kutolea huduma za hizo inasaidia kutambua hali ya mwenendo wa magonjwa yasiyo ya kuambiza na kuchukua hatua mapema kabla ya madhara kama vifo na ulemavu kutokea.
Hata hivyo, pamoja na mafanikio haya, ushirikiano wa wadau unahitajika ili kueneza elimu katika ngazi ya jamii juu ya mtindo salama wa maisha ili kuepuka magonjwa yasiyoambukiza, kujenga uelewa mpana wa jamii na kuielimisha jamii juu ya uchaguzi sahihi katika kulinda afya zao lengo likiwa ni kupunguza hatari kwa jamii.
Mwisho.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved