Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko, amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na Wakuu wa Wilaya kuhakikisha jamii inahamasishwa kutumia vyakula vilivyorutubishwa ili kukabiliana na changamoto ya udumavu na kuboresha afya ya wananchi.
Akiwaongoza wadau wa chakula katika kikao kazi kilichofanyika leo katika ofisi yake kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu urutubishaji wa chakula, RC Mrindoko amesisitiza umuhimu wa kutoa elimu kwa jamii juu ya lishe bora na virutubishi muhimu, sambamba na kuondoa dhana potofu kuhusu vyakula vilivyorutubishwa.
Pamoja na kuwa mkoa wa Katavi ni miongoni mwa wazalishaji wakuu wa mazao ya chakula nchini, hali ya lishe bado hairidhishi. Mkoa unaendelea kuchukua hatua madhubuti, ikiwa ni pamoja na kuongeza virutubishi kwenye chakula kupitia teknolojia ya usindikaji wa mazao. Katika hatua hiyo, Katavi imepokea mashine 20 mpya za usindikaji mazao kwa ajili ya kuongeza virutubishi kwenye vyakula, ambapo hadi sasa mashine 15 kati ya 359 zinazotumika kusaga unga zimeboreshwa kurutubisha chakula, sawa na asilimia 73 ya mashine zote.
Kaimu katibu tawala wa mkoa wa Katavi, Bw. Nehemia James, amebainisha kuwa mkoa unaendelea kutekeleza kampeni ya lishe kupitia mpango harakishi wa kupunguza udumavu. Mpango huo unajumuisha ushirikiano wa sekta mbalimbali na jitihada za uelimishaji kwa jamii nzima.
Wakati huohuo, Peter Kaja kutoka Wizara ya Afya ameeleza kuwa sehemu kubwa ya jamii inakula vyakula vilivyokobolewa au vya mizizi ambavyo kwa kawaida vina kiwango kidogo cha virutubishi. Amefafanua kuwa ukoboaji wa nafaka hupoteza zaidi ya asilimia 75 ya virutubishi, kwani vitamini na madini vingi hupatikana kwenye pumba na kiini cha nafaka.
Kikao hicho kimehitimishwa kwa kauli ya pamoja inayotaka wadau wote kuongeza kasi ya utoaji elimu ya lishe, kutumia teknolojia za kurutubisha chakula, na kushirikiana katika kuleta mabadiliko chanya ya kiafya kwa jamii ya Mkoa wa Katavi.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Postal Address: Box 235, Mpanda -Katavi
Telephone: 025-2957108
Mobile:
Email: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Katavi RS . All rights reserved.