Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Bw. Albert Msovela, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo kwa hatua ya kujibu na kutekeleza kwa weredi maagizo yaliyotolewa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).
Akizungumza katika kikao maalum cha Baraza la Madiwani kilichoketi tarehe 19 Juni, 2025 kwa ajili ya kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/2024 pamoja na maagizo ya LAAC, Katibu Tawala amesema Halmashauri ya Nsimbo imekuwa kinara katika utekelezaji wa maagizo hayo kwa wakati, jambo linaloonesha uwajibikaji na utayari wa kuzingatia misingi ya utawala bora.
RAS Msovela Ameeleza kuwa pamoja na kuwepo kwa hoja, hatua zilizochukuliwa na halmashauri hiyo zinaonesha kuwa hoja hizo zingeweza kuepukwa endapo majibu yangewasilishwa kwa wakati, kwa ufasaha, na kwa vielelezo kamili. Hata hivyo, amesisitiza kuwa msingi wa mafanikio hayo unatokana na watumishi wa halmashauri hiyo kuzingatia sheria, taratibu na miongozo ya kazi, na hivyo kuna matarajio kuwa hoja zote zilizobaki zitapatiwa majibu sahihi kwa wakati.
Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa na Mkaguzi wa Ndani, Bw. Chambi Ngelela, Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo ilipokea hati inayoridhisha (Unqualified Opinion) kutoka kwa CAG. Taarifa hiyo imeeleza kuwa jumla ya hoja 19 kati ya zilizowasilishwa zimefungwa baada ya kupatiwa majibu ya kuridhisha, huku hoja 40 zikiwa bado hazijafungwa. Aidha, maagizo yote 6 yaliyotolewa na Kamati ya LAAC yamekamilika kutekelezwa.
Akihitimisha kikao hicho, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Nsimbo, Mhe. Halawa Charles Malendeja, amesema mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano wa karibu uliopo kati ya wataalamu wa halmashauri hiyo na viongozi wa kisiasa, jambo ambalo limeiwezesha halmashauri kusimamia vyema utekelezaji wa mipango na majukumu yake katika kipindi cha miaka mitano.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Postal Address: Box 235, Mpanda -Katavi
Telephone: 025-2957108
Mobile:
Email: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Katavi RS . All rights reserved.