Mratibu wa Mradi wa BEVAC, Bi. Flosia Vugo, kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi, wamefanya ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika kutembelea Chama cha Ushirika cha Mazao ya Nyuki na kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo cha usindikaji wa mazao ya nyuki. Kituo hicho kinatarajiwa kuwa nguzo muhimu ya kuongeza thamani ya mazao kama asali na nta, na kuchangia katika kuimarisha uchumi wa wakazi wa eneo hilo. Katika ziara hiyo, jumla ya ndoo 270 zilikabidhiwa kwa chama hicho ili kusaidia shughuli za uvunaji wa asali kwa kutumia njia bora na za kisasa.
Timu hiyo pia ilitembelea eneo la “Manzuki Darasa” ambalo limeandaliwa kwa ajili ya kutoa mafunzo ya nadharia na vitendo kwa wafugaji wa nyuki. Kupitia darasa hilo, wanakikundi hujifunza mbinu bora za ufugaji wa nyuki, utunzaji wa mizinga, na usindikaji wa mazao ya nyuki kwa kuzingatia viwango vya ubora.
Katika hatua nyingine, timu hiyo ilitembelea Kikundi cha Wasakatonge kilichopo Kata ya Sibwesa, ambacho kina jumla ya wanachama 17. Kikundi hicho kilikabidhiwa mizinga 57 ya kisasa, ikiwa ni juhudi za kuongeza uzalishaji wa asali na kuimarisha kipato cha wanakikundi. Hata hivyo, kikundi hicho kilibainisha changamoto kadhaa zinazoathiri utekelezaji wa shughuli zao, ikiwemo upungufu wa mavazi ya kinga kwa ajili ya kuvuna asali na ukosefu wa mashine ya kisasa ya kukamulia asali.
Afisa Mifugo wa Mkoa wa Katavi, Bw. Zidihery Mhando, aliwahimiza wanakikundi kutumia vyema fursa zinazotolewa na mradi huo kwa lengo la kukuza uzalishaji na kuongeza thamani ya mazao ya nyuki. Alisisitiza kuwa sekta ya ufugaji wa nyuki ni mojawapo ya maeneo yenye fursa kubwa ya kiuchumi, hasa kwa vijana na wanawake, na kwamba ushiriki wao kikamilifu katika miradi kama hii utaleta mabadiliko ya kweli ya kiuchumi na kijamii.
Mradi wa BEVAC unaendelea kuwa chachu ya maendeleo kwa wafugaji wa nyuki kwa kuwajengea uwezo wa kuzalisha kwa wingi, kuchakata kwa ubora, na kuuza mazao yao kwa faida, hivyo kuchangia kikamilifu katika kukuza uchumi wa kaya na taifa kwa ujumla.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Postal Address: Box 235, Mpanda -Katavi
Telephone: 025-2957108
Mobile:
Email: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Katavi RS . All rights reserved.