Mkuu wa mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko ametembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme na ujenzi wa vituo vya kupokea, kupoza na kusambaza umeme Inyonga chenye uwezo wa 15MVA katika eneo la Utende wilayani Mlele mkoani hapa.
Akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo na miradi ya kimikakati leo Mei 14, 2025 wilayani Mlele Mhe. Mrindoko amesema Mradi huo unatarajiwa kuanza kutumika ifikapo Mei 20, 2025 ambapo pamoja na kuondoa changamoto ya kukatika kwa umeme utaongeza ari ya uwekezaji kutokana na kuwa gharama za uendeshaji wa miundombinu ya uzalishaji inayotegemea umeme itapungua.
Picha: Mkuu wa mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko akizungumza baada ya kukagua Mradi wa Ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme na ujenzi wa vituo vya kupokea, kupoza na kusambaza umeme Inyonga chenye uwezo wa 15MVA katika eneo la Utende wilayani Mlele.
Mkoa wa Katavi unatekeleza mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msonyo wa kilovoti 132 kutoka Tabora hadi Katavi na ujenzi wa vituo vya kupokea, kupoza na kusambaza umeme katika vituo vya Ipole chenye uwezo wa 15MVA, Inyonga chenye uwezo wa 15MVA na Mpanda chenye uwezo wa 35MVA.
"Awali wawekezaji walikuwa na kikwazo cha umeme kwa sababu hakukuwa na kituo cha kupozea umeme katika mkoa wetu na sasa changamoto imeisha hivyo kila mwananchi awaze kuwekeza katika maeneo tofauti ili kuweza kujijenga zaidi kiuchumi,".
PICHA: Muonekano wa eneo la mradi wa kupokea, kupoza na kusambaza umeme Inyonga chenye uwezo wa 15MVA na Mpanda chenye uwezo wa 35MVA unaotarajiwa kuanza kutumika Mei 20, mwaka huu.
Ameongeza kuwa ni wajibu wa wananchi kuilinda na kuitunza miundombinu uliyojengwa ili isichakae mapema pamoja na kuwahakikishia wananchi kuwa serikali kupitia wakala wa umeme vijijini Rea imeendelea kufikisha huduma ya umeme katika maeneo na vijiji na sasa hudumia hiyo imefika katika vitongoji hivyo ni wajibu wa wananchi kutumua fursa hiyo kujiimarisha kiuchumi kupitia umeme katika vitongoji vyao.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa niaba ya meneja wa Tanescomkoa wa Katavi Mhandisi Dalali Lunyamila amesema mradi unatekelezwa na serikali kwa fedha za ndani ambapo gharama yake ni bilioni 164.15 ulioanza Septemba 2022 na unatarajiwa kukamilika Juni 2025 huku utekelezaji ukiwa umefikia 96%.
"Mradi huu mara baada ya kukamilika utawezeshaKuunganisha Mkoa wa Katavi na umeme wa grid ya Taifa.itawezesha wawekezaji wa ndani na nje kuwa na uhakika wa kupata umeme kwa maendeleo ya Viwanda, kilimo na matumizi ya kijamii pia mapato kwa shirika la umeme Tanzania yataongezeka kwa kuunganisha wateja wengi zaidi na hivyo kujikwamua kiuchumi". Amesema Lunyamila.
Mwisho.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Postal Address: Box 235, Mpanda -Katavi
Telephone: 025-2957108
Mobile:
Email: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Katavi RS . All rights reserved.