Katavi, Mei 20, 2025 — Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limeendesha mafunzo maalum ya siku mbili kwa Maafisa Utamaduni na Maafisa Biashara kutoka halmashauri zote za Mkoa wa Katavi, yakilenga kuwawezesha kutumia kwa ufanisi mifumo ya AMIS na TAUSI ambayo imeunganishwa kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa huduma kwa wasanii na wadau wa sekta ya sanaa.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Afisa Masoko Mkuu wa BASATA, Bw. Martine Mwambene, amesisitiza umuhimu wa matumizi sahihi ya mifumo hiyo ya kidigitali ambayo inalenga kurahisisha usimamizi wa shughuli za sanaa, kurasimisha sekta hiyo, pamoja na kuongeza mapato ya ndani ya halmashauri kupitia mikakati ya kisasa ya ukusanyaji.
“Mifumo ya AMIS na TAUSI ni nyenzo muhimu katika kuwasaidia maafisa wetu kuwahudumia wasanii, vikundi, taasisi, kampuni na wamiliki wa kumbi za burudani kwa ufanisi zaidi,” amesema Bw. Mwambene.
Kwa upande wake, Afisa Sanaa kutoka BASATA, Bw. Hassan Das, amehimiza maafisa hao kuhakikisha wanaratibu na kuwarasimisha wadau wote wa sanaa katika maeneo yao, hususan wamiliki wa miundombinu ya burudani kama kumbi za sherehe, starehe na maonyesho, kupitia mfumo wa AMIS.
Akitoa shukrani kwa niaba ya washiriki, Afisa Utamaduni wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, Bi. Tunele Eliya, amelipongeza BASATA kwa kuandaa mafunzo hayo, akieleza kuwa yamekuja wakati muafaka na yatawasaidia kuongeza ufanisi katika kusimamia shughuli za sanaa na biashara katika halmashauri zao.
Mafunzo hayo yamefanyika kuanzia Mei 19 hadi 20, 2025, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kitaifa wa BASATA wa kutoa elimu ya matumizi ya mifumo ya AMIS na TAUSI kwa maafisa wa serikali za mitaa kote nchini.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Postal Address: Box 235, Mpanda -Katavi
Telephone: 025-2957108
Mobile:
Email: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Katavi RS . All rights reserved.