Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Bw. Albert Msovela, ametoa wito kwa watumishi wa umma kuhakikisha wanazingatia weredi na kufuata sheria katika utekelezaji wa majukumu yao, ili kuondoa hoja zisizo na mashiko katika ripoti za ukaguzi kutoka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Ametoa angalizo kuhusu tabia ya baadhi ya watumishi kufanya kazi kwa mazoea, hali ambayo imekuwa ikisababisha hoja nyingi za ukaguzi.
Ameeleza kuwa hoja zinazojitokeza kutokana na uzembe na kutokuheshimu sheria, kama vile kufanya manunuzi bila kutumia risiti halali za EFD, zinaepukika kabisa iwapo watumishi watafuata sheria kikamilifu. Amehimiza kuwa wakuu wa idara wanapaswa kuwajibika moja kwa moja katika kujibu hoja hizo, hatua ambayo itasaidia kuondoa uzembe na kuboresha huduma kwa wananchi.
Katika baraza maalum la madiwani lililoketi leo Juni 17, 2025, kwa ajili ya kupitia na kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali katika Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, CPA Kasea Lyoba kutoka Ofisi ya CAG Amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika imefanikiwa kupata hati safi ya ukaguzi kwa mwaka huo, ambapo jumla ya hoja 38 ziliibuliwa na mkaguzi. Kati ya hizo, hoja 18 zimehusu utendaji wa Halmashauri na 20 zimehusu usimamizi wa miradi ya maendeleo na mifuko mbalimbali. Aidha, hoja 16 kutoka miaka ya nyuma bado zimesalia, na hivyo kufanya jumla ya hoja zote kuwa 54.
Katika hatua ya utekelezaji, Menejimenti ya Halmashauri imeweza kutekeleza hoja 32 kati ya 54 kikamilifu na kupendekezwa kufungwa, huku hoja 22 zikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Akimhitimisha kikao hicho, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Mhe. Hamad Mapengo, kwa niaba ya baraza la madiwani, ameushukuru uongozi wa mkoa pamoja na menejimenti ya halmashauri kwa ushirikiano mzuri uliowezesha utekelezaji mzuri wa majukumu katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Postal Address: Box 235, Mpanda -Katavi
Telephone: 025-2957108
Mobile:
Email: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Katavi RS . All rights reserved.