Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi, amekutana na wananchi wa eneo la Western, sehemu iliyopo ndani ya Kitongoji cha Luhafwe, iliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji na yenye ukubwa wa hekta 46,000 (sawa na ekari 115,000), katika Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, mkoani Katavi. Lengo la mkutano huo limekuwa kusikiliza kero za wananchi na kuweka mikakati ya kutatua mgogoro wa ardhi unaolikumba eneo hilo.
Katika mkutano huo wa hadhara, Waziri Ndejembi ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejikita katika kuhakikisha haki inatendeka kwa kila mwananchi bila upendeleo. Amesisitiza kuwa maamuzi yote yanayochukuliwa katika eneo hilo yanazingatia maslahi mapana ya wananchi na kulinda amani ya jamii.
Waziri Ndejembi amewahimiza wananchi kuendelea na shughuli zao za kilimo katika maeneo waliyonayo kwa sasa, hadi suluhisho la kudumu kuhusu umiliki wa ardhi litakapopatikana. Aidha, amekemea ongezeko la kaya mpya katika eneo hilo, akibainisha kuwa hatua hiyo inaweza kuongeza ugumu wa kupata suluhisho la mgogoro uliopo. Ametoa maelekezo kuwa wakazi wapya wanaotaka kuingia katika eneo hilo wafahamishwe kuhusu hali halisi na waelekezwe kutafuta maeneo mengine ya makazi.
Katika kuhakikisha mgogoro huo unapatiwa ufumbuzi wa haraka, Waziri Ndejembi amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Mhandisi Anthony Sanga, kuunda timu maalum ya usuluhishi itakayochunguza suala hilo na kuwasilisha ripoti ya mapendekezo ndani ya wiki tatu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko, amemwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika kufuatilia uwepo wa vitongoji visivyotambulika katika eneo hilo, tofauti na Kitongoji cha Luhafwe ambacho ndicho kinachotambulika rasmi. Pia amesisitiza kuwa mihuri feki inayodaiwa kutumika itambuliwe na ikabidhiwe kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ndani ya siku tatu.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved