Mkuu wa Mkoa wa Katavi,Mhe. Mwanamvua Mrindoko, ameagiza kusimamishwa kazi watumishi wanne wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, kupisha uchunguzi wa utata wa matumizi ya Sh milioni 300 za ujenzi wa mradi wa Hospitali ya Wilaya ya Nsimbo.
Maagizo hayo ameyatoa 17 Septemba 2022 mara baada ya kufanya ziara ya kukagua ujenzi wa hospitali hiyo, ambapo baada ya kupokea Taarifa ya Matumizi ya fedha za Ujenzi wa Hospitali hiyo alibaini utata katika matumizi ya Shilingi Milioni 300.
Waliosimamishwa kazi ni pamoja na Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, Mkuu wa Idara ya Afya, Ofisa Mipango pamoja na mkaguzi wa ndani kwa kumdanganya kuhusu matumizi ya fedha hizo.
Pia amemuelekeza mkaguzi wa ndani wa Mkoa, pamoja wataalam wengine waliopo chini ya Katibu Tawala wa Mkoa, ndani ya siku saba kukagua Sh milioni 300, namna zilivyotumika, huku akitoa siku nyingine 30 kukagua miradi yote inayotekelezwa katika Halmashauri hiyo, ikiwemo vituo vya afya, shule na vituo vya tozo.
“Hii inaanza kunipa wasiwasi kwamba inawezekana hata hiyo miradi mingine kuna mambo ambayo hayaendi vizuri,” amesema RC Mrindoko.
Ameiagiza TAKUKURU Mkoa wa Katavi kukagua kwa undani mradi mzima wa hospitali ya Wilaya Nsimbo, ili kubaini ubadhirifu uliofanyika kuanzia matumizi ya fedha, ubora wa mradi, ununuzi wa vifaa na thamani zake na endapo watabaini wabadhirifu hatua kali za kisheria zichukuliwe.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Jamila Yusuf alimwambia mkuu wa Mkoa kuwa, Kamati ya Usalama Wilaya, baada ya kufuatilia matumizi ya Sh milioni 300, waliambiwa kiasi cha sh mil 210 zimetumika katika matumizi mengine nje na eneo lililokusudiwa, hivyo wakamuagiza mkurugenzi kufuatilia fedha hizo zilitumika vipi, lakini hakupata majibu.
“Hii milango unayoiona yote ilikataliwa na aliyekuwa Waziri wa Tamisemi, Ummy Mwalimu, hata kuridhia shilingi milioni 300 itoke kwa ajili ya kufanya umaliziaji ni pamoja na kutengeneza milango, ambayo unaiona hadi leo bado ipo, mimi ninachojua hiyo fedha haikutumika,” alisema DC Jamila.
Hata hivyo imeonekana katika ukaguzi wa ujenzi wa mradi huo, kwa nyakati mbalimbali baina ya Kamati ya Usalama ya Wilaya, Mganga Mkuu wa Mkoa pamoja na Mkuu wa Mkoa wote walipokea taarifa zisizofanana.
“Sisi tulivyokuja na kamati yako iliyokuja kukuwakilisha, maelezo tuliyopewa na uliyopewa wewe leo ni tofauti kabisa, sasa sielewi aliyedanganywa kati yetu ni nani, lakini nadhani umedanganywa wewe mheshimiwa Mkuu wa Mkoa,”alisema DC Jamila
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved