Katika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yatakayofanyika kimkoa tarehe 5 Machi 2025, wanawake wa mkoa wa Katavi wameungana katika zoezi la upandaji miti katika Shule ya Sekondari Mtemi Beda, Manispaa ya Mpanda. Zoezi hilo limebeba dhamira pana, likilenga si tu utunzaji wa mazingira, bali pia kuchochea uhamasishaji wa lishe bora kwa familia kama njia mojawapo ya kutokomeza lishe duni mkoani Katavi.
Akizungumza wakati wa shughuli hiyo, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Bi. Fidensiana Mwanakulya, ameeleza kuwa upandaji miti, hasa miti ya matunda na lishe, ni hatua muhimu katika kuhakikisha upatikanaji wa chakula chenye virutubisho vya kutosha kwa familia. Amesisitiza kuwa jamii inapaswa kutambua umuhimu wa mimea katika kuboresha afya, hususan kwa watoto na wanawake wajawazito, ambao mara nyingi hukumbwa na changamoto za lishe duni.
Pamoja na kuhimiza suala la lishe bora, Bi. Fidensiana amewataka wanawake kuwa karibu na watoto wao kwa kuhakikisha wanazungumza nao mara kwa mara kuhusu changamoto wanazokutana nazo katika maisha yao ya kila siku. Ameeleza kuwa malezi bora na mawasiliano ndani ya familia ni msingi wa kizazi chenye afya bora na maadili mema.
"Wanawake wana nafasi kubwa ya kulea kizazi chenye afya njema na kinachojitambua. Tusitumie muda wetu mwingi kwenye shughuli za nje na kusahau kuwapa watoto wetu malezi mazuri. Tuwaelekeze kuhusu lishe bora, afya, na maadili ili kuwajenga kuwa watu wenye manufaa kwa jamii," amesema Bi. Fidensiana.
Katika kuhitimisha hotuba yake, Bi. Fidensiana amewataka wanawake wa Katavi kushiriki kikamilifu katika shughuli zote za kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, huku akisisitiza umuhimu wa mshikamano katika kujenga jamii yenye afya na maendeleo.
Maadhimisho haya yanatarajiwa kuleta mijadala na shughuli mbalimbali zitakazolenga kuinua nafasi ya wanawake katika maendeleo ya jamii, huku suala la lishe bora likipewa msisitizo maalum kama njia ya kuhakikisha familia zenye afya na ustawi.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved