11 Novemba 2022,
Wakandarasi wa Barabara Mkoani Katavi wametakiwa kufanya kazi kwa weledi pamoja na kuzingatia masharti yaliyopo katika mikataba baina yao na Serikali ili thamani ya fedha iweze kuonekana.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Katavi Bi.Mwanamvua Hoza Mrindoko katika hafla ya utiaji saini mikataba ya ujenzi baina ya Wakala wa Barabara za Miji na Vijijini Nchini TARURA pamoja na Wakandarasi watakaotekeleza kazi za ujenzi,ukarabati na matengenezo ya miundombinu ya Barabara mkoani humo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 iliyofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Mpanda.
Jumla ya mikabata 6 imesainiwa yenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 1.5 kati ya TARURA na wakandarasi wa ujenzi wa barabara mkoani Katavi ikiwa ni asilimia 40 ya Bajeti ya Mwaka wa fedha 2022/2023.
"Tarura kwa Mwaka huu wa fedha 2022/2023 imetengewa Bajeti ya shilingi 14,293,366,636 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 30 kati ya miradi hiyo miradi 19 utiaji wake saini ulishuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Sulhu Hassan 14 Agosti 2022 jijini Dodoma ammbayo ilikuwa na thamani ya Shilingi 6,646,859,525 ambapo leo hii tumeshuhudia utiaji saini mikataba 6 yenye thamani ya shilingi 1,522,411,920 kati ya TARURA na Wakandarasi wa Ujenzi wa Barabara"Alisema Mkuu wa Mkoa Bi.Mrindoko.
Mkuu wa Mkoa Bi. Mrindoko amewataka TARURA mkoani Katavi kushirikiana na TANESCO ,RUWASA na MUWASA kuhakiki miundombinu iliyopo kwenye hifadhi za barabara na kuiondoa kwa wakati ili kuepusha ucheleweshaji wa miradi na usumbufu kwa wananchi kukosa huduma.
Aidha Bi Mrindoko amewasisitiza Wakandarasi hao kutoa kipaumbele cha ajira za muda zinazotokana na miradi kwa Wananchi wa maeneo husika paamoja na kuwalipa malipo yao kwa wakati ili Wananchi wa maeneo husika waweze kunufaika na fursa za Miradi hiyo katika maeneo yao.
Awali akitoa taarifa ya mikataba inayosainiwa, meneja wa TARURA mkoa wa Katavi mhandisi Innocent Mlay amesema wanategemea kujenga barabara mpya za lami zenye urefu wa km 3.73,kufungua barabara mpya km198,ujenzi wa Makalvati 182 na ujenzi wa barabara za changarawe zenye urefu wa km 155.16.
Naye Mwenyekiti wa umoja wa wakandarasi mkoa wa Katavi Juma Hassan Lumbwe amewataka wakandarasi waliotia saini mikataba hiyo kufanya kazi kwa kuzingatia viwango na kuisoma mikataba hiyo vizuri ili kuepusha migongano wakati wa utekelezaji wa miradi ya Serikali.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved