Njombe, Januari 30, 2025
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua H. Mrindoko, akiwa ameongozana na Wakuu wa Wilaya na wataalamu, ametekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kufanya ziara ya mafunzo mkoani Njombe. Ziara hii imelenga kujifunza mbinu bora za kupunguza udumavu, tatizo linaloendelea kuathiri Mkoa wa Katavi kwa kiwango kikubwa, ikiwa juu ya wastani wa kitaifa wa asilimia 32.2%.
Katika ziara yake ya Julai 2024, Rais Samia alieleza kuwa Mkoa wa Njombe umefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kupunguza udumavu na aliagiza viongozi wa Mkoa wa Katavi kujifunza kutoka kwa wenzao wa Njombe. Kwa mujibu wa Mhe. Mrindoko, ziara hii ni mwanzo wa ushirikiano wa karibu kati ya mikoa hii miwili, siyo tu katika sekta ya lishe, bali pia katika nyanja nyingine za kiuchumi, kijamii, na kiutalii. Amesisitiza kuwa ni fursa muhimu kwa wataalamu kutoka Katavi kubadilishana uzoefu na kujenga ushirikiano wa kudumu kwa ajili ya maendeleo ya mikoa hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, amekubali na kuunga mkono wazo la ushirikiano huu, akieleza kuwa mashirikiano haya yanaweza kupanuka zaidi kwenye sekta ya elimu, akitoa wazo la kuanzisha mitihani ya pamoja kwa wanafunzi wa darasa la saba, kidato cha pili na cha nne. Alisema kuwa hatua hiyo itachangia kuinua viwango vya taaluma na kukuza mshikamano kati ya mikoa hii miwili.
Ziara hii inatarajiwa kubadilisha mtindo wa utekelezaji wa afua za lishe katika Mkoa wa Katavi, kwa kutumia mbinu zilizofanikiwa katika Mkoa wa Njombe. Hivyo, ushirikiano huu utaleta manufaa makubwa kwa wananchi wa Katavi, ikiwa ni pamoja na kupunguza kiwango cha udumavu, kuimarisha afya na ustawi wa jamii, na kuchochea maendeleo katika sekta mbalimbali.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved