Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko, ameutaka Umoja wa Waendesha Bodaboda mkoani humo kuhakikisha hauhusiki na vitendo vya uvunjifu wa amani, bali uwe sehemu ya kulinda utulivu kwa kutoa taarifa kwa vyombo husika pindi wanapobaini dalili za machafuko katika maeneo yao ya kazi.
Akiwa mgeni rasmi katika mkutano mkuu wa umoja huo uliofanyika leo, Juni 5, 2025, mkoani Katavi, Mkuu wa Mkoa amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na kundi hilo la vijana kwa lengo la kuwawezesha kutekeleza majukumu yao katika mazingira salama na yenye heshima. Aidha, ametoa wito kwa viongozi wa umoja huo kuhakikisha wanawaongoza wanachama wao kwa haki, bila upendeleo wala ubaguzi.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa amewahamasisha waendesha bodaboda kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, sambamba na kuhamasisha vijana wenzao kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mchakato huo muhimu kwa mustakabali wa taifa. Amesisitiza kuwa ushiriki wa vijana katika uchaguzi ni wajibu wa kizalendo na mchango mkubwa kwa maendeleo ya demokrasia.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Waendesha Bodaboda Mkoa wa Katavi, Bw. Isack Daniel Joseph, amepongeza ushirikiano unaoonyeshwa na Serikali na kuahidi kuwa umoja huo utaendelea kuwa mlinzi wa amani mkoani Katavi. Aidha, amesema kuwa vijana wa bodaboda wamejipanga kuhamasisha wenzao kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kama sehemu ya kuwajibika kwa jamii na taifa.
Kwa upande wake, Katibu wa umoja huo, Bw. Daniel Vagas Sanga, akisoma risala mbele ya mgeni rasmi, amesema kuwa viongozi wamefanikiwa kufungua ofisi ya umoja wa waendesha bodaboda itakayorahisisha utendaji wa shughuli mbalimbali. Aidha, amesema kuwa wamefanikiwa kuandaa rasimu ya katiba ya umoja, ambayo kwa sasa inatumika kama mwongozo mkuu wa uendeshaji wa shughuli za kila siku.
Katika risala hiyo, Serikali pia imeshukuriwa kwa kuwezesha utoaji wa mikopo ya pikipiki 70 kupitia asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri, inayotolewa kwa makundi maalum, hatua iliyosaidia kuimarisha ajira kwa vijana na kuchochea uwajibikaji
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved