Kikao Kati ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi na Viongozi wa TABEDO Kujadili Maendeleo ya Ufugaji Nyuki Tanzania.
Leo, Januari 2, 2025, kikao muhimu kimefanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi kati ya Mkuu wa Mkoa, Mhe. Mwanamvua Mrindoko, na viongozi wapya wa Chama cha Kuendeleza Ufugaji Nyuki Tanzania (TABEDO). Kikao hicho kimekuwa na dhima ya kuwatambulisha viongozi wapya wa TABEDO pamoja na kuwasilisha malengo na mikakati yao ya kuimarisha sekta ya ufugaji wa nyuki nchini.
Viongozi wa TABEDO wamemuomba Mkuu wa Mkoa kushirikiana na Halmashauri zote za Mkoa wa Katavi kuhakikisha wanachama wa chama hicho wanapata msaada wa pamoja na kuhakikisha vikundi vyote vya wafugaji wa nyuki ndani ya mkoa vinajumuishwa rasmi kama wanachama wa TABEDO.
Rc Mrindoko, akizungumza katika kikao hicho, amesema kuwa Mkoa wa Katavi bado una fursa kubwa ya kuendeleza ufugaji wa nyuki kama shughuli ya kibiashara yenye manufaa kwa wananchi. Amebainisha kuwa mkoa umejipanga kuhakikisha sekta hiyo inapata kipaumbele cha juu, na ameongeza kuwa yapo maeneo mengi yanayoweza kutumika kuimarisha ufugaji wa nyuki kwa tija kubwa.
Aidha, ameongeza kuwa viongozi wa TABEDO wanapaswa kujipambanua kwa wadau wao wa chini, hususan wafugaji wa nyuki, na kuhakikisha wanajenga mnyororo wa thamani wa mazao ya nyuki kama asali na nta. Mheshimiwa Mrindoko kupitia kikao hicho kutoa wito kwa wawekezaji na wadau mbalimbali wenye nia njema ya kuwekeza katika sekta hiyo, akisisitiza kuwa Mkoa wa Katavi una uwezo mkubwa wa kuendeleza ufugaji wa nyuki na shughuli za uchakataji wa mazao hayo.
Ametoa hakikisho kwamba serikali ya mkoa itashirikiana kwa karibu na TABEDO na wadau wengine kuhakikisha sekta ya ufugaji nyuki inakua na kuchangia maendeleo ya kiuchumi kwa mkoa na taifa kwa ujumla.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved