Leo Januari 03, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko, amefanya ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo katika mkoa huo. Ziara hiyo imelenga kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa viwango vya ubora unaotakiwa, ndani ya muda uliopangwa, na kwa manufaa ya wananchi wa Katavi.
Miradi Aliyotembelea1. Ujenzi wa Shule Mpya ya Kanda ya Magharibi (Katavi Boys): Shule hii inayojengwa chini ya mpango wa uboreshaji wa elimu ya sekondari (SEQUIP) imelenga kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu bora. Mkuu wa Shule ya Sekondari Kasokola, Mwl. Gervas Gwakisa, amesema ujenzi wa shule ulianza tarehe 05 Oktoba, 2024 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Machi 04, 2025.“Mnamo Juni 22, 2024, tumepokea shilingi bilioni 4.1 kutoka OR-TAMISEMI kwa ajili ya mradi huu. Hadi sasa, utekelezaji umefikia asilimia 17.61, na fedha zimehifadhiwa kwenye akaunti ya shule kuhakikisha usimamizi wa uwazi na uwajibikaji,” amesema Mwl. Gwakisa.
2. Ukarabati wa Barabara na Ujenzi wa Mifereji Mpanda Mjini:Mradi huu umehusisha ukarabati wa barabara za lami Mpanda Mjini, ujenzi wa mifereji ya mawe, na matengenezo ya muda maalum ya Barabara ya Mtapenda yenye urefu wa kilomita 4.7. Mradi huu una lengo la kuboresha usafiri, kuimarisha uchumi wa eneo hilo, na kudhibiti mafuriko.
3. Mradi wa Wodi ya Wazazi na Jengo la Upasuaji Kituo cha Afya Kazima:Katika kituo hiki, Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa ya Mpanda, Dkt. Limbu Mazoya, amesema kuwa serikali imetoa shilingi milioni 250 mnamo Septemba 02, 2024 kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya wazazi na jengo la upasuaji. Hadi sasa, shilingi milioni 40.210 zimetumika, na ujenzi umefikia hatua ya boma.“Mradi huu ni muhimu kwa kuboresha huduma za afya ya uzazi na upasuaji kwa wakazi wa eneo hili,” amesema Dkt. Mazoya.
Maelekezo ya RC Mrindoko kwa Wakandarasi na Viongozi,
Baada ya kukagua miradi hiyo, Mhe. Mrindoko ametoa wito kwa wakandarasi kuhakikisha wanakamilisha kazi zao kwa viwango vinavyotakiwa na kwa kuzingatia muda wa mkataba.“Wakandarasi, mnapochukua kazi za serikali, msizichukulie kama miradi ya nyumbani. Hakikisheni mnatekeleza kwa uaminifu na kwa mujibu wa mikataba,” amesema.Aidha, Mhe. Mrindoko ametoa maelekezo kwa wakuu wa wilaya kuhakikisha doria zinazofanyika katika misitu na mapori tengefu hazihusishi ufyekaji wa mazao ya wananchi.“Ni marufuku kufyeka mazao ambayo tayari yamekua. Waliohusika na kitendo hicho wanapaswa kuwapatia wananchi mbegu ili wapande mazao mengine katika maeneo yanayoruhusiwa,” amesema kwa msisitizo.HitimishoMhe. Mrindoko amehitimisha ziara yake kwa kusisitiza umuhimu wa ushirikiano, uwajibikaji, na uwazi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Ameahidi kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote ili kuboresha maisha ya wananchi wa Katavi.
Ziara hiyo imeonyesha dhamira ya serikali ya kuhakikisha maendeleo endelevu yanapatikana kwa wakati na kwa kiwango cha juu, huku changamoto zikichukuliwa kama fursa za kuboresha mfumo wa utekelezaji.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved