Viongozi wa Serikali pamoja na Wadau mbalimbali wa Elimu Mkoani Katavi wametakiwa kujipanga ili kuhakikisha kuwa wanaondoa kabisa changamoto mbalimbali zinazoikabili Sekta ya Elimu Mkoani Katavi.
Rai hiyo imetolewa Septemba 9, 2022 na Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe Mwanamvua Hoza Mrindoko katika hafla ya uzinduzi wa ugawaji wa miongozo ya uboreshaji wa sekta ya Elimu iliyofanyika katika Ukumbi wa Idara ya maji Manispaa ya Mpanda ikiwakutanisha wadau mbalimbali wa Elimu wakiwemo Viongozi mbalimbali wa Wilaya ya na Halmashauri.
Mhe.Mrindoko ameeleza kikaoni hapo kuwa Licha ya Mafanikio makubwa ya Mkoa wa Katavi katika Sekta ya Elimu yaliyochangiwa zaidi na hatua mbalimbali ambazo Serikali ya awamu ya sita imezichukua katika kuboresha Sekta ya Elimu Mkoani Katavi ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya Elimu Kama vile Ujenzi wa madarasa na mengine mengi, bado jitihada za dhati za wadau mbalimbali wa Elimu zinahitajika katika kuhakikisha kuwa changamoto mbalimbali zinazoendelea kuikabili sekta ya Elimu Katavi zinapatiwa ufumbuzi na kumalizwa kabisa.
“Sisi kama Mkoa bado tunayo changamoto ya Wanafunzi kukatiza masomo kutokana na sababu mbalimbali na wengine kushindwa kuendelea na masomo kutokana na Jamii inayowazunguka.Tunaendelea kupata watoto wanaochaguliwa kujiunga na Kidato cha kwanza na wanashindwa kuendelea.Katika hili kila mdau ana wajibu wa kuhakikisha kuwa hatuna mdondoko wa wanafunzi na kwamba ni wajibu wetu kama wadau kuhaikisha kuwa watoto wote wanaojiunga na kidato cha kwanza wanamaliza kidato cha nne”Alisema Mhe.Mrindoko.
Mhe.Mrindoko pia amebainisha kuwa ipo changamoto ya baadhi ya wazazi kuwazuia watoto kuendelea na masomo kutokana kisingizio cha kukosa uwezo na hivyo kuwataka Vingozi Ngazi zote kuhakikisha kuwa inafuatilia changamoto hiyo nbva kuchukua hatua stahiki kwa wale wote wanaozuia watoto kwenda Shuleni kwa kisingizio cha kukosa fedha ikiwa ni pamoja na kutoa Elimu kwa Jamii juu ya madhara ya kutowapeleka watoto Shuleni.
Mhe.Mrindoko amewaelekeza wakuu wa Wilaya Mkoani Katavi kuhakikisha kuwa wanatatua changamoto mbalimbali zinazoikabili Sekta ya Elimu ikiwemo kushughulikia changamoto ya wazazi wanaozuia watoto kuendelea na masomo kwa kuchukua hatua stahiki
Akifafanua zaidi kuhusu miongozo hiyo Afisa Elimu Mkoa wa Katavi Dr.Elipidius Baganda amesema miongozo hiyo imeelezea namna mbalimbali ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili Sekta ya Elimu ambapo kupitia miongozo hiyo itakayowafikia wadau wote wa Elimu katika ngazi ya Jamii itasaidia kwa sehemu kubwa kutoa muongozo wa namna ya kukabiliana na kuondoa changamoto mbalimbali zinazoikabili Sekta ya Elimu ndani ya Mkoa wa Katavi lengo likiwa ni kuinua ubora wa Elimu Mkoa wa Katavi
Nao wadau mbalimbali walioshiriki katika uzinduzi huo wa Ugawaji wa Miongozo hiyo katika ngazi ya Mkoa wameeleza kuwa Wazazi na walezi ni wadau muhimu hivyo ni muhimu wazazi kushirikiana kwa karibu na Wazazi ili kuhakikisha kuwa watoto wanapata Elimu kama inavyotakiwa
“Kama wazazi watawawekea watoto misingi mizuri mpaka wanafika shuleni watakuwa na misingi mizuri lakini ushirikiano wa Walimu na wazazi ni kitu muhimu na endapo hakutakua na ushirikiano basi changamoto hizo zilizoainishwa katika miongozo zitaendelea hivyo ni jukumu letu kama wazazi na walimu kudumisha ushirkiano kwa ustawi mzuri wa watoto .” alisema Mwalimu Sabas Korongo.
Elizabeth Madenge Mwalimu kutoka Wilayani Mpimbwe amemshukuru Rais Samia kwa namna ambavyo anatoa kipaumbele katika Sekta ya Elimu na kwamba amefarijika kupata miongozo ambayo inatoa dira ya namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali katika Sekta ya Elimu.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved