RC KATAVI AWATAKA WANANCHI KUDUMISHA AMANI
Amani ndiyo msingi mkubwa wa maendeleo duniani. Binadamu au taifa lolote duniani haliwezi kuwa na maendeleo yoyote yale bila kuwa na amani.
Amani huvutia wawekezaji, hujenga mazingira ya uzalishaji, huwawezesha watu kufanya shughuli mbali za kijamii na kiroho mfano kuabudu. Kumbe amani ni muhimu siyo tu katika kuwezesha maendeleo katika jamii bali katika kudumisha maendeleo endelevu.
Hakuna serikali duniani isiyopenda amani na utulivu kwa wananchi wake na mipaka yake. Daima serikali huwahimiza wananchi wake kuimarisha na kudumisha amani kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wenyewe na taifa kwa ujumla.
Serikali duniani zimeweka sheria, kanuni na taratibu ili kuhakikisha kuwa amani na utulivu vinadumishwa kwa wananchi na mipaka yake.
Tanzania ni miongoni mwa serikali duniani zilizojiwekea sheria, kanuni na taratibu kwa ajili ya kuhakikisha kuwa amani na utulivu vinadumu nchini na kwa wananchi wake.
Mkoani Katavi, kiongozi mkuu wa mkoa huo, Mhe. Mwanamvua Mrindoko anajitokeza mbele ya vyombo vya habari kuwapongeza wakristo wote mkoani kwake na taifa kwa ujumla kwa kuendesha mfungo wa kwaresma na kuingia katika sikukuu za pasaka kwa amani na utulivu mkubwa.
Mhe. Mrindoko anasema mkoa umeendelea kuwa salama, tulivu na shwari kutokana na ushirikiano mkubwa ambao wananchi wake wameutoa kwa vyombo vya dola katika kudumisha amani na utulivu.
Katika maadhimisho ya sikukuu za pasaka, kiongozi huyo anatoa maelekezo na tahadhari mbali mbali katika kipindi chote cha maadhimisho ya sikukuu na baada ya sikukuu hizo.
Mhe. Mrindoko anawaonya wananchi wote waliojipanga kufanya fujo na ghasia kwa wakristo wote watakao kuwa kwenye ibada kuwa wasithubutu kufanya hivyo kwa kuwa watajutia kupanga hivyo.
Amesema vyombo vya dola vimejipanga kuhakikisha kuwa usalama na utulivu vinaendelea kuwepo sehemu zote za ibada, majumbani na katika kumbi zote za starehe.
Mhe. Mrindoko amesema vyombo vya dola vitafanya doria na misako sehemu mbali mbali ili kuhakikisha kuwa amani inatamalaki katika mkoa wakati wote wa sikukuu na baada ya sikukuu
Kuhusu watoto na wanafunzi, Mhe Mrindoko amepiga marufuku kwa watoto au wanafunzi kwenda kwenye kumbi za starehe na badala yake wapelekwe kwenye maeneo ya wazi ambapo hakuna uwezekano wa kutokea ajali yoyote
Ameonya wazazi watakaokiuka agizo hilo, vyombo vya dola vitawachukulia hatua za kisheria ili kukomesha tabia hiyo
Pamoja na marufuku hiyo, kiongozi huyo amewatahadharisha wanaoendesha vyombo vya moto kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zote za usalama barabrani ili kuepusha ajali zisizo za lazima katika kipindi na baada ya sikukuu.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved