Pichani:Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe.Mwanamvua Mrindoko akizungumza na mmoja wa Wafanyabiashara wa duka katika kata ya makanyagio wakati wa ukaguzi wa utekelezaji Zoezi la Uwekaji wa vibao vya namba katika Nyumba.
Na: John Mganga-Katavi- RS
Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe.Mwanamvua Mrindoko ametoa onyo kwa Wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara ya vyuma chakavu kujihadhari na ununuzi wa vyuma vitokanavyo na miundombinu ya Serikali.
Mhe.Mrindoko ametoa onyo hilo kufuatia uwepo wa Taarifa za upotevu wa baadhi ya Vibao vya chuma vya anuani za makazi katika baadhi ya mitaa katika Manispaa ya Mpanda.
Akizungumza Wananchi wa Kata ya Makanyagio mara baada ya kukagua utekelezaji wa zoezi endelevu la uwekaji wa vibao vya anuani za makazi Mhe.Mrindoko amesema ni jukumu la kila Mwananchi kulinda miundombinu ya Serikali kwa kuwa Serikali imewekeza fedha nyingi katika miundombonu hiyo.
Amesema hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayebainika kuhujumu miundombinu hiyo ya anuani za makazi huku akisisitiza kuwa Mfanyabiashara yoyote wa vyuma chakavu atakayebainika kujihusisha na ununuzi wa vyuma vitokanavyo na miundombinu ya serikali hatua kali zitachukuliwa dhidi yake ikiwa ni pamoja na kufungiwa kufanya biashara hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Mpanda Bi.Sophia Kumbuli amekiri kuwepo kwa upotevu wa baadhi ya vibao vya anuani za makazi katika baadhi ya maeneo ambapo ameeleza kuwa kama Manispaa wamechukua hatua ya kugharamia ununuzi wa Vibao hivyo na kuviweka katika baadhi ya maeneo yaliyokumbwa na kadhia hiyo.
Bi.Kumbuli ametoa wito kwa Wananchi wa Manispaa ya Mpanda kutoa ushirikiano kwa Serikali kulinda miundombinu hiyo ambayo ina faida kubwa kwa Wananchi.
Nae Mstahiki Mea wa Manispaa ya Mpanda Mhe.Haidary Sumry ameipongeza Manispaa ya Mpanda kwa kutekeleza zoezi hilo kwa umakini mkubwa huku akiishukuru Serikali ambapo amesema ni muhimu kwa Viongozi kuendelea kuwaelimisha Wananchi kuhusu umuhimu wa zoezi la Anuani za Makazi pamoja na faida zake.
Kwa Upande wao baadhi Wananchi wa Makanyagio wameshauri Serikali kuendelea kutoa elimu kwa Wananchi juu ya faida za Mfumo wa anuani za makazi ili waweze kutumia fursa hiyo kurahisisha shughui za kiuchumi.
Zoezi la uwekaji mfumo wa anuani za makazi Mkoani Katavi limekamilika kwa Asilimia 100 ambapo licha ya changamoto kadhaa maendeleo ya zoezi endelevu la uwekaji wa vibao katika Mitaa linaendela vizuri.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved