Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Hoza Mrindoko, amehimiza wafanyabiashara na wadau wa maendeleo kuongeza ubunifu katika bidhaa na huduma wanazozalisha, ili kuongeza ushindani wa kibiashara na kuchochea ukuaji wa uchumi mkoani Katavi.
RC Mrindoko ametoa msimamo huo wakati akitembelea mabanda ya washiriki kutoka Katavi katika maonesho ya kilimo ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya. Ametumia fursa hiyo kusisitiza kuwa ubunifu na matumizi ya teknolojia ni nyenzo muhimu kwa mkoa huo kufikia maendeleo ya haraka.
Katika ziara hiyo, RC Mrindoko ameambatana na viongozi mbalimbali wakiwemo Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Mheshimiwa Onesmo Buswelu, Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Mheshimiwa Jamila, na Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Mheshimiwa Alhaji Majid, pamoja na wakurugenzi wa halmashauri, wakuu wa idara na wataalamu kutoka mkoani Katavi.
Aidha, Mkuu huyo wa mkoa ametangaza fursa za uwekezaji zinazopatikana mkoani Katavi, akieleza kuwa sekta za kilimo, ufugaji, biashara, usafirishaji na mawasiliano zinahitaji wawekezaji zaidi kutokana na mazingira mazuri ya miundombinu na utayari wa serikali kushirikiana na sekta binafsi.
Katika maelezo yake, amebainisha maeneo maalum ya uwekezaji ndani ya Wilaya ya Tanganyika, yakiwemo Bandari ya Karema inayofungua fursa za kibiashara kupitia Ziwa Tanganyika, biashara ya kaboni, shughuli za uvuvi, pamoja na kilimo na ufugaji ambapo zaidi ya hekta 46,000 zimetengwa rasmi kwa ajili ya wawekezaji.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Mheshimiwa Onesmo Buswelu, ameeleza kuwa wilaya yake imejipanga vizuri kuweka mazingira rafiki kwa wajasiriamali na wawekezaji wa ngazi zote. Ameongeza kuwa Wilaya ya Tanganyika imenufaika na zaidi ya shilingi bilioni 500 kutoka Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa ajili ya miradi ya maendeleo inayowanufaisha wananchi wa Katavi.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved