Taasisi ya Afya Ifakara (IHI) katika jitihada zake za kupambana na Ugonjwa wa Malaria Nchini imeutambulisha Mradi wa miaka 5 utakaosaidia mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Malaria Mkoani Katavi.
Akiutambulisha Mradi huo katika ukumbi wa Katavi Resort Manispaa ya Mpanda Mwakilishi kutoka Taasisi ya Afya Ifakara Dkt.Dustan Bishanga ameeleza kuwa Mradi huo unaojulikana kama Malaria Survailance Activity unafadhiliwa na Shirika la USAID kupitia mfuko wa Rais wa Marekani wa kupambana na Malaria PMI (President Malaria Initiative) ambapo zaidi ya Bilioni 40 zitatolewa na Mfuko huo kwa ajili kutelekeza Mradi huo.
Dkt.Bishanga amesema Mradi huo utajikita zaidi katika Uboreshaji wa huduma za Malaria,Kujenga uwezo kwa watumishi wa wanaohusika na utoaji wa huduma za Ugonjwa Malaria,Utoaji wa Elimu kwa Wananchi pamoja na Uimarishaji mifumo ya Taarifa za Ugonjwa Malaria itakayosaidia kujua mwenendo wa Ugonjwa wa Malaria Mkoani Katavi.
Akizungumza katika kikao cha Utambulisho wa Mradi huo Katibu Tawala Mkoa wa Katavi Bw.Hassan Abas Rugwa amesema Mradi huo umekuja kwa wakati muafaka kwa kuwa Mkoa wa Katavi ni miongoni mwa mikoa yenye kiwango cha juu cha maambukizi ya Ugonjwa wa Malaria kwa Asilimia 7.1
Katibu Tawala Rugwa amesema ni muhimu kwa Wataalamu wa Afya pamoja na wadau wote katika Mapambano ya Malaria kuelekeza jitihada kubwa katika kuhakikisha kuwa mradi uliotambulishwa unatekelezwa kwa ufanisi mkubwa ili uweze kuleta matokeo chanya ya kuondoa Malaria jambo litakalosaidia kuchochea ukuaji wa Uchumi Mkoani Katavi.
Bw.Rugwa ameeleza kuwa uwepo wa Ugonjwa wa Malaria kunachangia kwa kiasi kikubwa kuathiri uchumi katika Sekta mbalimbali Nchini ikiwemo sekta ya Utalii kwa kuwa Watalii wengi hawapendelei kutembelea maeneo ambayo yametajwa kuwa na kiwango cha juu cha maambukizi ya Ugonjwa wa Malaria.
Aidha Katibu Tawala Rugwa ametoa wito kwa wataalamu wa Afya Mkoani Katavi kuendelea kutoa elimu ya kutosha kwa Wananchi juu ya njia mbalimbali za kupambana na Malaria ikiwemo Matumizi ya Vyandarua,Usafi wa Mazingira,Matumizi ya Viuadudu, pamoja na kuhamasisha matumizi ya Teknolojia ya kisasa ya matumizi ya Vifaa vya kielektroniki vya kuangamiza Mbu.
Kwa Upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Katavi Bw.Omari Sukari ameishukuru Taasisi ya Afya Ifakara kwa kusapoti mapambano ya malaria Mkoani Katavi
Ameeleza kuwa licha ya jitihada mbalimbali za Serikali kupambana na malaria bado maambukizi ya ugonjwa wa malaria yamekua yakiongezeka ambapo kwa sasa bado kama Mkoa wanaendelea na jitihada za Ugawaji wa Vyandarua pamoja na utoaji wa Elimu ya namna ya kutokomeza malaria husuani kwa watoto chini ya Umri wa miaka 5 pamoja na Akina mama wajawazito.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Mpanda Bi Sofia Kumbuli ameishukuru Taasisi ya Afya Ifakara kwa kutoa sapoti kubwa itakayosaidia kwa sehemu kubwa mapambano ya Malaria Mkoani Katavi ambapo kwa niaba ya Wakurugenzi wa Halmashauri Mkoani Katavi ameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza mradi huo.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved